Wana-CCM walioshindwa uchaguzi wa mitaa waenda kortini

Katibu Mkuu wa CCM, Abdulhaman Kinana.
Makada 10 waliogombea   uenyeviti wa vitongoji, vijiji na mitaa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Halmashauri ya Wilaya Tarime, mkoani Mara, wamekata rufaa katika Mahakama ya Wilaya Tarime kupinga matokeo yaliyowapa ushindi wapinzani wao.

Wengi wao wanadai kuwa  kulikuwa na udanganyifu katika uchaguzi huo kutokana na  karatasi za kupigia kura  kuzidi idadi ya watu waliojiandikisha, kuwapo  karatasi bandia za kura,  ubabe na vitisho kutumika wakati wa upigaji kura.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Katibu wa CCM Wilaya ya Tarime, Barnabas Nyerembe,  alisema:

Licha ya kwamba licha ya kuhamishiwa Tarime baada ya uchaguzi wa Serikali za mitaa  uliofanyika Desemba 14, 2014,  baadhi ya waliokuwa wagombea uenyekiti wa mitaa, vitongoji na vijiji kupitia CCM wamempelekea madai yao ya kupinga matokeo ya uchaguzi huo mahakamani.

Alisema wagombea hao wamechua hatua hiyo ili haki iweze kutendeka kutokana na uchaguzi kutokuwa huru na haki.

Aliongeza kuwa makada hao wanadai kuwa mchakato wa kutangaza matokeo haukuzingatia mamalamiko kutoka pande zote mbili.

Nyerembe aliwataja waliokata rufaa na kufungua kesi  katika Mahakama ya Wilaya Tarime kupinga matokeo yaliyowapa ushindi waliokuwa wagombea wenzao ni Julius  Nyang’era kutoka kijiji cha Nyarero na Godfrey Francis  kutoka Mtaa wa Mwangaza.

Wengine ni Prisca Kibasa wa Mtaa wa Kibasa, Mwita Makuri kutoka kijiji cha Mrito, Jacob Chacha Ryoba, Kenguru Tagaya mtaa wa Starehe na William Werema kutoka kijiji cha Kwisarara.

Wajumbe watatu waliopinga matokeo na kukata rufaa ni Paschal Musomi, John Chege na Pili Mambo.

Kesi hizo ziko kwa Hakimu wa Mahakama ya Wilaya, Adrian  Kilimi.

Alisema: “Chama Cha Mapinduzi kinawaomba waliokuwa  wagombea kupitia  CCM walioshindwa katika wilaya hii ya Tarime na wenye ushahidi na vielelezo waweze kuviwakilisha mapema kabla ya Jumatano Januari 15,  kwani ndiyo siku ya mwisho ya kukata rufaa kwa wenye malalamiko.”
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post