Kesi ya kina Mdee kutolewa uamuzi leo

Halima Mdee.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo itatoa uamuzi kuhusu hoja za wakili wa Utetezi, Peter Kibatala, ya kuomba wateja wake kufutiwa shtaka la pili katika kesi kutotii amri halali ya Jeshi la Polisi na kufanya mikusanyiko isivyo halali kwa lengo la kwenda Ikulu inayomkabili Mbunge wa Jimbo la Kawe, Halima Mdee na wenzake wanane.
Mbali na Mdee, washtakiwa wengine ni Rose Moshi (45), Renina Peter, Anna Linjewile (48), Mwanne Kassim (32), Sophia Fangel (28), Edward Julius (25), Martha Mtiko (27) na Beatu Mmari (35), wote wakazi wa Dar es Salaam.
Wakili Kibatala aliiomba mahakama hiyo iwafutie washtakiwa shtaka la pili katika hati ya mashtaka akidai kuna mapungufu kisheria kwa kuwa hakuna vifungu vya sheria vilivyoainisha shtaka hilo.

Upande wa mashtaka uliiomba mahakama kutupilia mbali ombi hilo ukidai hakuna madhara  au upungufu kisheria katika shtaka hilo na kwamba si lazima kila kifungu kitajwe huku ukisistiza kungekuwa na madhara iwapo mashtaka ama shtaka hilo lingekuwa halipo au haliingiliani na kifungu chochote cha sheria.

Hakimu Mkazi, Janeth Kaluyenda, aliihairisha kesi hiyo kutokana na kutokamilisha  utoaji wa uamuzi mdogo wa ombi la upande wa utetezi.

Desemba 16, 2014 Mdee na wenzake walisomewa maelezo ya awali ya na Mawakili wa Serikali, Ahmed Salim na Wakili Mwandamizi, Tumaini Kweka, walidai mbele ya Hakimu, Kaluyenda kwamba washtakiwa hao walikamatwa katika Mtaa wa Ufipa wakiwa wamebeba mabango na kukana mashtaka yote.

Mawakili hao walidai washtakiwa hao walikaidi amri halali ya Polisi iliyowataka kutawanyika baada ya wafuasi hao kutaka kutembea kwenda kumuona Rais Jakaya Kikwete kwa ajili ya kupinga Katiba Inayopendekezwa.

Wakili Salim alidai baada ya wafuasi hao kukaidi kufuata amri hiyo, iliwalazimu polisi kutumia nguvu kuwatawanya kwa kosa la kufanya fujo.Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa, Oktoba 4, 2014 washtakiwa wakiwa Mtaa wa Ufipa, bila kuwa na uhalali walikiuka amri halali ya kutawanyika iliyotolewa na Mrakibu wa Polisi (SP), Emmanuel Tillf, kwa niaba ya Jeshi la Polisi.

Ilidaiwa kuwa washtakiwa hao walitenda kosa hilo kinyume cha kifungu cha 124 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Katika shtaka la pili, washtakiwa hao wakiwa eneo hilo, walifanya mkusanyiko usio halali kwa lengo moja la kutembea kwenda Ofisi ya Rais, huku wakijua ni kinyume cha sheria.
 
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post