Baadhi
ya Wanafunzi 84 wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) wakiwa chini ya ulinzi
kwa tuhuma za kuhamasisha uvunjifu wa amani Chuoni hapo na kufanya
maandamano haramu kutoka Chuoni kuelekea katika Ofisi mbalimbali za
viongozi wa Serikali zilizopo mjini Dodoma leo.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma inawashikilia wanafunzi 84 wa chuo
Kikuu UDOM kwa tuhuma za kuhamasisha uvunjifu wa amani Chuoni na kufanya
maandamano haramu kutoka Chuoni kuelekea katika Ofisi mbalimbali za
viongozi wa Serikali zilizopo Dodoma Mjini leo tarehe 14.01.2015 majira
ya 05:30hrs.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa
Polisi DAVID MISIME – (SACP) ameeleza kuwa chanzo cha wananfunzi hao wa
programu maalum ya Diploma ya Ualimu kufanya uhalifu huo ni kikao
walichofanya wananfunzi hao tarehe 13.01.201 wakidai kuongezewa posho ya
chakula na kwamba hata kiasi ambacho wanapewa wamechelewa kupewa.
Hata hivyo uongozi wa Chuo uliwaeleza kuwa wenye mamlaka ya
kuzungumzia swala la kuongezewa posho ni Bodi ya Mikopo na siyo chuo.
Hivyo walitakiwa kufuata taratibu za kuwasilisha madai yao. Pia
walielezwa kuwa hundi kwa ajili ya fedha za posho zao zimeshasainiwa na
kuwasilishwa Benki ili waweze kuanza kupewa posho zao.
Wanafunzi hao hawakuridhika na usiku wakaanza kuhamasishana kufanya
maandamano jambo ambalo ni kosa kisheria. Wanafunzi hao wamehojiwa
kulingana na ushahidi ambao umekusanywa na wamefikishwa mahakamani kwa
kosa la Kufanya Maandamano yasiyo na kibali.
Viongozi waliohamasisha uvunjifu huo wa sheria baadi wamekamatwa na
baadhi wanaendelea kutafutwa ili nao waweze kuchukuliwa hatua stahiki.
Ushahidi uliokusanywa unaonyesha jinsi viongozi hao wameshiriki
kuhamasisha kupitia vikao rasmi na visivyo rasmi, katika vikundi, kupita
katika mabweni na kutuma sms.
Kamanda MISIME ametoa wito kwa Wanafunzi hao kutumia taratibu
zilizowekwa na Serikali na Chuo kuwasilisha malalamiko yao ngazi kwa
ngazi na siyo kufanya vitendo vya kuvunja sheria ambavyo
vitawasababishia kukamatwa. Endapo watafanya hivyo wasije kulaumu mtu
kwani hatua zitachukuliwa kulingana na Sheria inavyoelekeza ikiwa ni
pamoja na kufikishwa mahakamani.
إرسال تعليق