Kama ilivyozoeleka katika jamii
zetu za Kiafrika, baba ndiye nguzo ya familia ingawa katika huduma za
afya zinamweka mama na mtoto katika makundi maalumu katika kupata huduma
za afya.
Kupitia kona hii nitawaletea mfululizo wa makala zinazotoa ufahamu kuhusu matatizo mbalimbali ya kiafya kwa wanaume.
Wanaume wanahitajika kuwa na
tahadhari kuhusiana na afya zao, kwani unapowalinganisha na wanawake na
watoto, wao wako katika hatari ya kupata magonjwa mbalimbali.
Jambo ambalo hata halihitaji
utafiti wa kisomi, jaribu kupita katika maeneo ya burudani utagundua
robo tatu ya wateja ni wanaume.
Wanaume ndiyo “wanaopiga maji”
na kuvuta sigara kwa wingi na ndiyo wanaokuwa na uchaguzi wa tabia
hatarishi za kupata matatizo ya kiafya.
Tabia hatarishi ni kama vile kuwa na wapenzi wengi na upande mwingine ndiyo wanaowindwa zaidi na madada wanaofanya ukahaba.
Kutokana na uwezo wao wa kufanya
kazi na kujiingizia kipato kikubwa, wanaume wana uwezo wa kufanya
chochote kwa kufanya ushawishi wa anasa mbalimbali.
Uwezo walio nao huweza kuwafanya
wale vyakula kiholela bila kuzingatia kanuni za afya, ulevi kupindukia,
hivyo kuwa na uzito mkubwa uliokithiri au kunenepa sana.
Maumbile ya kiume na mfumo mzima
wa homoni zake, unamfanya mwanaume kuwa na mrundikano zaidi wa mafuta
ndani ya mwili katika viungo kama moyo, ini na figo. Hii ni tofauti na
mwanamke.
Hii ni moja ya sababu za wanaume
wengi kuwa na magonjwa ya moyo, mishipa ya damu, kisukari, maradhi sugu
ya figo, kiharusi, magonjwa ya akili na unene ulipitiliza.
Wanaume pia huwa na maradhi
ambayo huwapata wao pekee. Magonjwa hayo ni kama vile saratani ya tezi
dume na kiasi kidogo cha homoni ya kiume iitwayo kitabibu
‘testosterone’.
إرسال تعليق