Kama wengi wetu tunavyofahamu, damu ya binadamu imegawanyika
katika makundi makuu manne; A, B, AB, na O. Lakini pia makundi haya
kutokana na aina ya mfumo kinga wa Rh.
Mfumo huo wa RH yamegawanyika zaidi katika makundi
madogo kama vile kundi A (hasi), kundi A (chanya), kundi B (hasi),
kundi B (chanya), kundi AB (hasi), kundi AB (chanya), kundi O (chanya)
na kundi O (hasi). Binadamu yeyote lazima awe mojawapo ya makundi hayo.
Historia inaonyesha kuwa makundi haya ya damu
yaligundulika kutokana na jitihada za wataalamu wa tiba za kujaribu
kuokoa maisha ya wagonjwa waliokuwa wanapungukiwa damu.
Wataalamu hawa walipojaribu kuwaongezea watu damu
za wanyama au za binadamu wengine, mara nyingi walipoteza maisha na hii
ilichochea udadisi ili kujua zaidi kuhusu damu.
Tofauti za makundi yetu ya damu zinatokana na urithi wa vinasaba vinavyotofautiana kutoka kwa wazazi wetu.
Kwa mujibu wa J.R. Storry na M.L. Olsson katika
utafiti wao uliochapishwa katika jarida la kisayansi la Immunohematology
toleo la 25 mwaka 2009, vinasaba vya urithi vinaweza kuamua kuwepo kwa
tofauti za makundi ya damu kwa kutengeneza mifumo tata na iliyo tofauti
ya kinga dhidi ya magonjwa katika ukuta wa nje wa chembechembe nyekundu
za damu.
Hata hivyo kila kundi lina faida na hasara zake
pale tunapoyahusisha makundi ya damu na uwezekano wa kuchangia kutokea
kwa magonjwa au kutukinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza na magonjwa
ya kuambukiza.
Kwa kipindi cha takribani miaka 20 sasa,
wanasayansi wa maswala ya afya na tiba wamekuwa wakifanya tafiti
mbalimbali kuhusiana na uwezekano wa makundi mbalimbali ya damu
kuchochea au kuzuia utokeaji wa magonjwa kadhaa ambayo binadamu anaweza
kuyapata.
Ushahidi wa tafiti nyingi umeonyesha kuwepo kwa mahusiano ya karibu baina ya makundi ya damu na hali ya afya ya mtu.
Katika utafiti wa hivi karibuni ulio ongozwa na
N.A. Zakai wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Vermont nchini Marekani na
kuchapishwa katika jarida la kitabibu lijulikanalo kwa jina la Journal
of Thrombosis and Haemostasis toleo la 12(4) la mwaka huu, ilibainika
kuwa watu wenye kundi la damu la AB wanakabiliwa na uwezekano mkubwa wa
kupata ugonjwa wa kiharusi.
Katika utafiti mwingine wa mwaka 2006 ulioongozwa
na Siripen Kalayanarooj wa Taasisi ya Afya ya Watoto ya Malkia Sirikit
ya nchini Thailand (Queen Sirikit National Institute of Child Health,
Bangkok, Thailand ), pia ilibainika kuwa watu wenye kundi la damu la AB,
wako katika hatari kubwa ya kupata homa ya Dengue kuliko watu wengine.
Utafiti huo ulichapishwa kwenye jarida la magonjwa ya kuambukiza (The Journal of Infectious Diseases) toleo la 195(7).
- Mwananchi
- Mwananchi
Post a Comment