Baada ya kutangaza kumtema katika kikosi chao cha
Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, uongozi wa Yanga umesema kwamba
utamshitaki aliyekuwa kipa wao, Juma Kaseja, katika Kamati ya Nidhamu ya
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Akizungumza jana na gazeti hili, Ofisa Mawasiliano wa Klabu ya
Yanga, Jerry Muro, alisema kuwa kutangaza kumtema ilikuwa ni jambo la
kwanza na kinachofuata ni kumshitaki kipa huyo katika kamati hizo
zinazosimamia soka Tanzania.
Muro alisema pia Yanga imepanga kumshitaki Kaseja katika mahakama
za kawaida za nchi kwa sababu kuna baadhi ya makosa aliyofanya
hayahusiani na soka peke yake.
"Tunajipanga kuandaa malalamiko kwenda katika Kamati ya Nidhamu na
Kamati ya Sheria na Haki za Wachezaji, hatutaishia kumtema tu," alisema
Muro.
Aliongeza kuwa Yanga inachukua maamuzi hayo ili kuhakikisha kwamba
wachezaji pia wanaheshimu mikataba yao na isionekane kwamba klabu ndiyo
zimekuwa na tabia ya kuonea wachezaji.
Alisema baada ya kuondolewa katika mashindano ya Kombe la
Mapinduzi, Yanga leo itafanya mazoezi mepesi kwenye uwanja wao wa Kaunda
na kesho itaelekea Bagamoyo kuweka kambi.
Aliongeza kuwa sekretarieti iko katika hatua za mwisho za kuandaa
barua na kuipeleka TFF ili kuomba ruhusa ya kuelekea Zambia kushiriki
kwenye mashindano maalumu waliyoalikwa.
Yanga ilitangaza kumuacha Kaseja na kueleza kuwa inamdai kipa huyo
wa zamani wa Simba na timu ya Taifa (Taifa Stars) fidia ya Sh. milioni
340.
Meneja wa Kaseja, Abdulfatah Saleh, hakuweza kupatikana jana ili
kueleza msimamo wa mchezaji huyo ambaye yuko nje ya timu tangu mwaka
jana.
CHANZO:
NIPASHE

Post a Comment