Jamii imetakiwa kukubali ushiriki wa watu wenye ulemavu katika shughuli za kisiasa ikiwa ni pamoja na uongozi.
Katibu Mtendaji kutoka Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wenye Ulemavu
Zanzibar (UWWZ), Mwandawa Khamis, alisema watu wenye ulemavu wamekosa
ushirikishwaji wakionekana hawana nafasi katika uchaguzi wa kisiasa.
Aliyasema hayo wakati wa mkutano wa siku moja kati ya taasisi yake
na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) na UN Women Mkoa wa
Mjini Magharibi, Unguja.
Alisema mara nyingi nafasi za uongozi kwa kundi hilo zimekuwa ni za
viti maalum, lakini pia huangushwa wakati wa uchaguzi wa ndani ya
vyama.
Akitoa mfano wa uchaguzi wa mwaka 2010, alisema wanawake 11 wenye
ulemavu walijitokeza kugombea nafasi maalum zikiwamo za Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kutoka jumuiya yake ambapo hakuna aliyeshinda.
“Safari hii pia tumejipanga kugombea hadi nafasi za jumla ila
sambamba na hilo, tunahitaji jamii ibadilike ili itukubali kuwa wagombea
na kutuchagua kutokana na uwezo wetu siyo ulemavu wetu,” alisema.
Aliitaja jamii kuwa ni pamoja na wapiga kura katika hatua ya
uchaguzi wa ndani ya vyama, wapiga kura wa jumla na zaidi viongozi wa
kisiasa.
Naye mjumbe wa umoja huo, Saada Hamad Ali, alisema ushiriki wa watu
wenye ulemavu ni muhimu ili watetee kundi hilo linalokabiliwa na
changamoto nyingi zaidi.
Alisema kundi hilo linakabiliwa na ukatili mkubwa wa kijinsia na ambapo kwa asilimia kubwa kesi zake hufelishwa mahakamani.
Akitoa mfano, alisema kwa mwaka 2011 hadi 2014, zaidi ya kesi 115
ziliripotiwa lakini ni kesi mbili tu ndizo zilizopata haki mahakamani.
CHANZO:
NIPASHE

Post a Comment