Ikiwa imepita siku moja baada ya Mwenyekiti wa
askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) waliokosa ajira, George Mgoba,
kueleza jinsi alivyotekwa na kuteswa, wenzake wameibuka na kutaka
uchunguzi huru ufanyike kubaini sindano aliyochomwa kama ilikuwa na
sumu.
Mgoba ambaye alitekwa Jumatatu iliyopita na kutelekezwa kwenye moja
ya mapori mkoani Pwani, juzi ndugu zake walilazimika kumhamishia
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi akitokea Amana.
Akizungumza na NIPASHE jijini Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti
wa vijana hao, Parali Kiwango, alisema wanachotaka kujua ni sumu
aliyochomwa mwenzao na hatua zitakazochukuliwa.
Kiwango alisema kwa sasa wanataka kusimamia matibabu ya mwenzao na
kuchagua sehemu ya kumfanyia uchunguzi ili kuzuia serikali kuficha
baadhi ya ripoti.
Alisema mpaka sasa haijafahamika sindano hiyo ilikuwa na nini.
“Tunachotaka sisi kama viongozi na polisi tushirikiane kuteua
hospitali huru ya kuchunguza afya ya mwenzetu, lakini polisi wamekuwa
wakituzuia kushiriki kwenye hilo tunaona kunausiri unaoendelea,”alisema.
Akielezea kuhusu hali ya Mgobba, alisema bado siyo nzuri na kwamba
tayari alishachukuliwa sampuli mbalimbali kwa ajili ya uchunguzi.
“Tumeambiwa vipimo vinafanywa nje ya Muhimbili, lakini hatujui ni
hospitali ipi, ubinafsi huu tulianza kuuona kutoka Hospitali ya Tumbi
tulipotaka kumchukua walitukatalia walitugomea na wao kutudanganya
wanampeleka hospitali kumbe walimleta kituo cha Polisi Kati kwa
mahojiano zaidi,” alisema.
KUTOA TAMKO LEO
Kiwango alisema leo wamekusudia kutoa tamko rasmi kuhusu mwenendo
mzima wa sakata hilo kutokana na baadhi ya viongozi wa serikali kukwepa
kusema ukweli kuhusu madai yao ya ajira.
Alisema kwa sasa maisha yao yapo hatarini baada ya kuwapo kwa watu wanaowafuatilia majumbani kwao na kila wanapokwenda.
“Kwa jumla hatupo salama tunawaomba Watanzania waelewe hivyo, sisi tunadai haki yetu halali,” alisema.
CHADEMA CHAZUNGUMZIA
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
Tanzania Bara, John Mnyika alisema mara zote jeshi la polisi limekuwa
likisema uongo dhidi ya matukio ya utekaji na uteswaji wa watu.
Alikumbusha baadhi ya matukio ya utekwaji na uteswaji na
ushambuliwaji wa baadhi ya watu ambao ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Madaktari, Dk. Steven Ulimboka, kutekwa na kushambuliwa kwa Mwenyekiti
wa Jukwaa la Wahariri na Mhariri wa Kampuni ya magazeti ya New Habari,
Absalom Kibanda, ambayo alisema hadi sasa Serikali imekuwa na
kigugumizi.
Mnyika alisema baada ya kupata taarifa dhidi ya tukio la mwenyekiti
wa vijana wa JKT, alipiga simu kwa jeshi la polisi ili kujua kiini
chake, lakini hawakumweleza ukweli.
Mbunge huyo wa jimbo la Ubungo aliihoji Ikulu kwa nini mambo yanayoihusisha ofisi hiyo yamekuwa yakisababisha watu kutekwa.
Pia aliihoji serikali kwa nini watekaji hao wamekuwa wakikihusisha
chama hicho na vitendo vyao vya kiutekaji kwa kuwahoji wahusika kama
wametumwa na Chadema au viongozi wake.
MIKOA YAUNGANA KUCHUNGUZA
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova,
aliliambia gazeti hili jana kuwa, upelelezi wa tukio hilo la kutekwa na
kuteswa kwa Mgoba, utahusisha mkoa wake wa kipolisi na mkoa wa Pwani.
Kamanda Kova alisema mikoa hiyo imekubaliana kufanya uchunguzi wa
pamoja wa kina kuhusiana na tukio hilo ambalo lilihusisha Dar es Salaam
alikotekewa mtu huyo na Pwani alikoteswa.
“Tumeanza uchunguzi na mara utakapokamilika basi tutaueleza Umma, tunaomba utulivu wakati hili likiendelea,” alisema.
Miongoni mwa madai ya vijana hao ni kupata ajira katika vikosi mbalimbali vya kijeshi kutokana na mafunzo waliyopatiwa.
mwisho

إرسال تعليق