JAJI Mkuu mstaafu, Augustino Ramadhani
--
JAJI Mkuu mstaafu, Augustino Ramadhani, ambaye jina lake limeanza
kutajwa kwenye kuwania Urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ametajwa
kutoa “mojawapo ya maamuzi ya hovyo kabisa” katika historia ya Mahakama
hapa nchini, Raia Mwema linafahamu.
Hata hivyo, mwanasheria mkongwe na mmoja wa wanasiasa maarufu nchini,
Mabere Marando, amemweleza Jaji Ramadhani kama mmoja wa wanasheria
wazuri hapa nchini.
Mahojiano na watu waliowahi kufanya naye kazi na usomaji wa nyaraka
mbalimbali zinazomhusu Jaji huyo, umeonyesha jaji huyo anachukuliwa kwa
namna tofauti katika tasnia ya sheria lakini kwenye jamii kwa ujumla
uadilifu, uungwana na ucha Mungu wake unaelezwa kama sifa zake kuu.
Jambo ambalo limeweka doa katika wasifu wa Ramadhani (70) ni kitendo
chake cha kutoa hukumu ya suala la mgombea binafsi ambapo alisema suala
hilo halipaswi kuamuliwa na Mahakama kwa vile ni la kisiasa na Bunge
ndilo linatakiwa kusimamia suala hilo.
Jaji Ramadhani alikuwa kiongozi wa benchi la majaji saba wa Mahakama ya Rufani ambayo ilikaa kujadili kesi hiyo ya mgombea binafsi ambayo kwa mara ya kwanza ilifunguliwa na Mchungaji Christopher Mtikila mwaka 1993. Katika hukumu hiyo ya Juni 17, 2010, Jaji Ramadhani ambaye ndiye aliyeiandika alisema;
Jaji Ramadhani alikuwa kiongozi wa benchi la majaji saba wa Mahakama ya Rufani ambayo ilikaa kujadili kesi hiyo ya mgombea binafsi ambayo kwa mara ya kwanza ilifunguliwa na Mchungaji Christopher Mtikila mwaka 1993. Katika hukumu hiyo ya Juni 17, 2010, Jaji Ramadhani ambaye ndiye aliyeiandika alisema;
“Katika kesi hii, suala la mgombea binafsi linafaa kushughulikiwa na Bunge ambalo ndilo lenye mamlaka ya kisheria ya kubadili Katiba na si Mahakama. “Uamuzi wa ama kukubali au kukataa kuanzisha utaratibu wa mgombea binafsi katika chaguzi zote unategemea na mahitaji ya kila jamii kutokana na historia yake. Hivyo, suala la mgombea binafsi si la kisheria bali ni la kisiasa,”ilieleza hukumu hiyo.
Akizungumzia kuhusu hukumu hiyo, mmoja wa mawakili maarufu hapa nchini,
Alex Mgongolwa, alisema hukumu hiyo ya suala la mgombea binafsi inatajwa
kuwa kama mojawapo ya hukumu za hovyo kabisa katika historia ya
Mahakama hapa nchini.
“Mimi ukiniambia ninakumbuka nini kwenye uongozi wa Jaji Augustino Ramadhani kama Jaji Mkuu nitakwambia kuhusu hukumu yake ya mgombea binafsi. Ile ni hukumu ambayo imetia doa heshima yake,”alisema Mgongolwa.
Majaji wengine ambao walishirikiana na Ramadhani kwenye hukumu hiyo ni
Benard Luanda, Sauda Mjasiri, January Msoffe, Nathalia Kimaro, Eusebia
Munuo na Mbarouk Salim Mbarouk Maamuzi hayo ya Mahakama ya Rufani
yalikosolewa na wasomi wengi wa taaluma ya kisheria; ambapo mmoja wao,
Profesa Gamaliel Mgongo Fimbo, alinukuliwa wakati huo akiuita ni
“disaster” (maafa).
Hata hivyo, aliyepigilia msumari wa mwisho kuhusu namna hukumu hiyo
ilivyokuwa na mushkeli alikuwa ni Jaji Mkuu mstaafu, Barnabas Samatta,
ambaye miezi mitano baada ya hukumu hiyo kutoka alitoa maoni yake.
Akizungumza katika Chuo Kikuu cha Ruaha Novemba 25 mwaka 2010, Samatta
aliichambua huku hiyo kwa mapana, na kueleza kwamba imeipunguzia nguvu
Mahakama na kuongeza nguvu kwa Bunge. Akiwasilisha mada iliyojulikana
kwa jina la Judicial Protection of Democratic Values (Mahakama na Ulinzi
wa Tunu za Demokrasia) ambayo Raia Mwema imefanikiwa kuona nakala yake,
Samatta aliileza kesi hiyo ya mgombea binafsi kama “Mojawapo ya kesi
muhimu zaidi za kikatiba katika historia ya Tanzania. Katika uamuzi wake
huo, Mahakama ya Rufani imeliepa jukumu la Mahakama la kutafsiri sheria
ambalo haliwezi kufanywa na chombo kingine chochote isipokuwa chenyewe.
“Suala la mgombea binafsi linagusa haki za msingi za wananchi. Haki ya kugombea, kama zilivyo haki nyingine za msingi, ni haki ambayo Mtanzania anazaliwa nayo na hawezi kunyang’anywa labda kwa sababu ambazo zimeelezwa kwenye Katiba,”aliandika Samatta.
Kwenye maelezo ya kesi hiyo, Jaji Ramadhani aliunga mkono maelezo ya
mmoja wa marafiki wa Mahakama, Profesa Palamagamba Kabudi, aliyenukuu
maelezo ya Profesa Conrad wa Ujerumani, kuwa “ hakuna hitimisho hadi
sasa la wapi zinapoishia haki za msingi”.
Samatta alifafanua kwamba Ramadhani na Kabudi hawakufafanua vizuri
kuhusu maelezo hayo ya Conrad kwa vile yamefafanuliwa vizuri katika
baadhi ya hukumu za kikatiba zilizoamuliwa nchini India na ambazo
alizinukuu katika maelezo yake. Katika mojawapo ya nukuu kuntu katika
hukumu ya Jaji Ramadhani, kwa kufuata ushauri huo wa Kabudi na Conrad,
Mahakama ya Rufani ilihoji; “ Suala hili la kudai haki za msingi
litaishia wapi? Leo wanadai mgombea binafsi, kesho watadai nini?”
Jaji Samatta ambaye wanasheria wanamsifu kama mojawapo ya majaji wakuu wanaoheshimika alijibu hoja hiyo kwa kusema;
“ Madai yataisha pale haki zote za msingi zitakapokuwa zimepatikana. Huwezi kumnyima mtu haki kwa madai kwamba akipewa haki hiyo, atadai na nyingine”.
Akimnukuu mojawapo ya majaji maarufu wa Ghana, Jaji Kayode, Samatta
aliandika; “If floodgates it entails, let there be one, once it is a
matter of fundamental right(Kama hili litasababisha mafuriko ya haki,
basi na yaje tu ali mradi suala linahusu haki za msingi”.
Akizungumzia hukumu hiyo, Marando alisema suala la mgombea binafsi
linategemea na maoni ya mtu kwani wanaopendelea mgombea binafsi wanaweza
kuwa na mtazamo tofauti na wasiopendelea suala hilo.
“Nimemfahamu Jaji Ramadhani kwa muda wa zaidi ya miaka 20. Ni mwanasheria mzuri sana. Hukumu zake nyingi zina maamuzi murua kabisa. “Hiyo ya mgombea binafsi inaweza kuwa isiwe kipenzi cha wengi lakini siwezi kuiita ya hovyo. Inategemea tu na mtazamo wa mtu kuhusu suala hilo,”alisema.
Hata hivyo, mmoja wa viongozi wastaafu wa Chama cha Wanasheria wa
Tanganyika (TLS) aliliambia Raia Mwema kwamba katika mojawapo ya
mikutano ya kuagana aliyofanya na chama hicho, Jaji huyo alieleza kwamba
uamuzi huo ulitokana na shinikizo walilopata kutoka serikalini hasa
ikizingatiwa kuwa hukumu hiyo ilitolewa katika mwaka wa uchaguzi.
Katika gazeti la Raia Mwema toleo lililopita, ilielezwa kwamba Jaji
Ramadhani ameibuka kama mojawapo ya kete za Chama Cha Mapinduzi (CCM)
katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, kutokana na kuwa na sifa mahususi
zinazohitajika, ingawa mwenyewe hajaonyesha nia. Sifa hizo ni uadilifu,
uaminifu kwa chama na serikali, Uzanzibari wake, Ukristo na weledi wake;
sifa ambazo inadaiwa baadhi ya wale ambao wanafahamika kutaka kumrithi
Rais Jakaya Kikwete kutoka Tanzania Bara hawana kwa sasa.
Mmoja wa waliokuwa wajumbe katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba
iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba walimweleza Jaji Ramadhani kama mtu
aliyekuwa akipendelea muundo wa serikali mbili kama ilivyo sasa ingawa
alikubaliana na mapendekezo ya Tume ya Serikali Tatu kwa sababu yalikuwa
ni ya wananchi.
“Hii ndiyo sababu humuoni akizunguka mikoani au kwenye vyombo vya habari kupinga Katiba Inayopendekezwa kama baadhi ya wajumbe na Jaji Warioba mwenyewe wanavyofanya.
“Yeye anaamini kwamba kazi waliyotumwa na serikali wameimaliza ingawa pia hakufurahishwa na namna serikali ilivyowatendea wajumbe baada ya kumaliza shughuli za tume.
“Kama ukiniuliza nikutajie watu wawili waliokuwa waumini wa mfumo wa serikali mbili kindakindaki ndani ya Tume ya Jaji Warioba nitakutajia Jaji Ramadhani na Dk. Salim Ahmed Salim,” alisema mjumbe huyo.
Jaji Ramadhani ndiye Mtanzania pekee aliyeweka rekodi ya kuacha kazi ya
Ujaji Mkuu wa Zanzibar na kwenda vitani wakati wa Vita vya Kagera
mwishoni mwa miaka ya 1970, ambapo alipigana vita hiyo kwa muda wa miezi
kumi. Ni katika maisha yake hayo ya jeshini ndipo alipopanda cheo hadi
kufikia kile cha Brigedia Jenerali ambacho ndicho alichostaafu akiwa
nacho.
Post a Comment