Zanzibar. Chama cha CUF kimesema hakihusiki na
bendera za Afro Shiraz Party(ASP) zinazoonekana katika mikutano yake ya
hadhara inayofanyika Unguja na Pemba.
Kupepea kwa bendera hizo kumeibua mjadala mkubwa miongoni mwa viongozi wa CCM visiwani humo.
Msimamo huo wa CUF umeleezwa na Mkurugenzi wa Haki
za Binadamu na Mawasiliano kwa Umma, Salum Abdallah Bimani baada ya
UVCCM Zanzibar kulalamika kuwa CUF kimekiuka sheria Namba 5 ya mwaka
1992 ya vyama vya siasa huku mamlaka zikifumbia macho suala hilo.
“Wanaopepeprusha bendera hizo ni Wazanzibari
wanaoguswa na sera pamoja na misingi ya ASP. CUF haihusiki na bendera
hizo,” alisema Bimani.
Alisema ni kweli bendera hizo zimekuwa
zikionekana kwenye mikusanyiko na mikutano ya hadhara inayoandaliwa na
CUF ila hubebwa na wananchi wenye hisia za kukiunga mkono ASP kisera,
kimsimamo na kihistoria.
Bimani alisema CUF kinaweza kuhusishwa na bendera
hizo iwapo zingekuwa zinapepea kwenye milingoti ya ofisi zake za matawi,
wadi, jimbo, mikoa au Taifa lakini kupeperushwa kwenye mikutano hakuna
uhusiano wowote na chama hicho.
Hata hivyo alisema Ofisi ya Msajili wa Vyama vya
Siasa ndiyo yenye mamlaka ya kusimamia sheria na si vyama vya siasa na
kumtaka Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar Shaka Hamdu Shaka kuacha
kuihusisha CUF na bendera hizo.
Kwa upande wake Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa
Zanzibar, Rajab Baraka alipoulizwa kuhusiana na madai ya UVCCM, alisema
ni kweli wamepokea malalamiko kuhusiana na kupeperushwa kwa bendera hizo
na tayari suala hilo limewasilishwa Makao Makuu ya Ofisi ya Msajili
jijini Dar es Salaam.
“Tayari tumelizungumza suala hilo na
kinachosubiriwa ni maamuzi ya kisheria baada ya wanasheria wetu
kulifanyia kazi na kulitolea ufumbuzi, uamuzi wake hauhitaji kukurupuka
ila lazima kuwe na tafakuri na hekima kabla ya kutoa maamuzi mazito,”
alisema Baraka.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za
UVCCM huko Gymkhana mjini Zanzibar, Shaka alisema CUF kimeamua kuleta
chokochoko za kisiasa ambazo zinaweza kuitingisha na kuzorotesha amani,
utulivu na maridhaino yaliofikiwa visiwani humu. “Kitendo cha kubeba
alama za chama chetu cha zamani ASP na kuzitumia kwenye mikutano yao ya
hadhara licha ya kuwa ni uvunjaji wa sheria lakini kinaweza kuibua
mitafaruku na mapigano yasiohitajika, tunaonya kwa mara ya mwisho
ikishindikana tutazilinda bendera zetu,” alisema Shaka.
Naibu huyo Katibu Mkuu wa UVCCM alisema
inashangaza Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kushindwa kuchukua hatua
za kisheria huku ikiridhia uvunjaji wa sheria.
“Kikundi kinachojiita mguu mbele, mguu nyuma
kinachotambuliwa na Katibu Mkuu wa CUF Seif Sharif Hamad hubeba bendera
na kuimba nyimbo za harakati za Mapinduzi ya Zanzibar, ZNP hakina
mnasaba na ASP, iweje CUF kitumie sera za ASP kilichozaa CCM,” alihoji
Shaka.
إرسال تعليق