Bosi Bandari amvimbia Sitta

Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta.
Siku moja baada ya Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, kutangaza kumsimamisha kazi kwa muda usiojulikana Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Madeni Kipande, Mkurugenzi huyo ameibuka na kueleza kuwa ameshangazwa na uamuzi huo kwa kuwa hakuwahi kuitwa kabla na Bodi ya Wakurugenzi wa TPA kuelezwa tuhuma hizo kama taratibu na sheria zinavyoelekeza.
 
Sitta alisema alimsimamisha kazi Kipande kutokana na tuhuma za kukiuka taratibu za zabuni pamoja na mahusiano mabaya na wateja wa mamlaka hiyo.
 
Akizungumza na NIPASHE jana jijini Dar es Salaam, Kipande alisema tuhuma zilizotolewa kwake siyo za kweli na wala hakuna taratibu zozote za zabuni zilizokiukwa kama ilivyoelezwa na Sitta.
 
“Sijaitwa na Bodi kuulizwa kabla kuhusu tuhuma zilizoelekezwa kwangu isipokuwa Waziri alikuja jana (juzi) na kusema anataka kikao cha Bodi kuzungumza na wajumbe,” alisema.
 
Kwa mujibu wa taratibu, Mkurugenzi wa TPA  ndiye Katibu wa Bodi, hivyo vikao vyote vya Bodi vinapaswa kuitishwa na yeye kujadili mambo yote yanayohusu TPA.
 
Kipande alisema kwa kuwa Waziri Sitta ameunda kamati kuchunguza tuhuma zilizoelekezwa kwake, ana imani kuwa kamati hiyo itatenda haki ili ukweli wa mambo aliyotuhumiwa ujulikane.
 
“Tumekutana katika kikao cha dharura cha Bodi ya Bandari kutokana na kuzingatia malalamiko ya sehemu mbalimbali kwamba taratibu za zabuni TPA hazikukaa sawa, zinaendeshwa katika namna ambayo hazileti imani, nampongeza Dk. Harrison Mwakyembe, alianza vizuri kushughulikia suala hili, lakini bado tatizo halijaisha,” alisema Sitta.
 
“Nimemsimamisha kazi kwa muda Kaimu  Mkurugenzi  Mkuu wa Mamlaka ya Bandari, Madeni Kipande kuanzia Februari 16, mwaka 2015,  ili kupisha uchunguzi unaohusu tuhuma mbalimbali zinazomkabili,” alisema na kuongeza:
 
“Tuhuma hizo ni pamoja na manung’uniko kuhusiana na ukiukwaji wa taratibu za manunuzi.”
 
Alisema TPA ni kituo muhimu cha uchumi wa nchi kwa sababu karibu asilimia 87 ya mapato yanatoka hapo, hivyo kunahitajika watu kufanya kazi kwa umakini na uadilifu zaidi.
 
Sitta alisema hapakuwapo na uwazi katika zabuni kiasi kwamba hata baada ya Bodi ya Zabuni kufanya maamuzi, kumekuwa na ucheleweshaji wa kutoa barua ya kuidhinisha zabuni hizo, hivyo kuleta taswira mbaya kwa serikali.
 
“Kwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Madeni Kipande, ndiye msimamizi mkuu wa masuala yote ya bandari kuanzia leo, namsimamisha kazi hadi hapo tume niliyoiunda kuchunguza masuala hayo itakapokamilisha kazi,” alisema.
 
Sitta alitangaza kamati aliyoiunda kuchunguza suala hilo kuwa ni Jaji mstaafu Agusta Bubeshi, ambaye atakuwa Mwenyekiti na Katibu wake ni mfanyakazi wa Wizara ya Uchukuzi, Deogratius Kasinda.
 
Wajumbe wengine ni Dk. Ramadhani Mlingwa, ambaye ni Mkurugenzi mstaafu wa Mamlaka ya Manunuzi ya Umma  (PPRA); Flavian Kinundo (Mkurugenzi mstaafu wa Masoko TPA; Hapiness Senkoro na Mhandisi Samson Luhigo, ambao ni wafanyakazi wastaafu wa TPA.
 
Alisema ameamua kuwateua wastaafu katika kamati hiyo ambayo itafanya kazi ya uchunguzi kwa wiki mbili kwa sababu watu hao hawahitaji cheo.
 
Baada ya uamuzi huo, Sitta amemteua Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Awadh Massawe, kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA.
 
Kipande aliteuliwa Agosti, mwaka 2012 na Dk. Mwakyembe ambaye alikuwa Waziri wa Uchukuzi, baada ya kuwasimamisha kazi vigogo sita wa TPA akiwamo Mkurugenzi Mkuu, Ephraem Mgawe, kutokana na tuhuma mbalimbali za wizi.
 
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

أحدث أقدم