Bundi wa majanga ameendelea kuwanyemelea mawaziri,
safari hii wakitaka kichwa cha Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro
Nyalandu na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William
Lukuvi.
Nyalandu alituhumiwa kwa uzembe wa kushindwa kutoa tangazo kwenye
gazeti la Serikali (GN), ambalo limesababisha Serikali kupoteza mapato
ya zaidi ya Sh. bilioni 80.
Aliyedai kichwa cha Nyalandu ni mbunge wa Kigoma Kaskazini
(Chadema), Zitto Kabwe, akitaka Waziri huyo amwandikie Rais barua ya
kujiuzulu wadhifa wake, kwa kuikosesha serikali mapato hayo. Zitto
alitoa hoja hiyo wakati akichangia mjadala uliohusu taarifa ya
utekelezaji ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira na ile ya Kilimo,
Mifugo na Maji, zilizowasilishwa bungeni jana.
Alisema kuwa tangu wiki iliyopta wabunge walikuwa wakilalamika
kutopatikana kwa mapato ya Serikali kwenye miradi mbalimbali ya
maendeleo, lakini kumbe kuna mapato yanayopotea kutokana na uzembe wa
Waziri huyo.
Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Kamati ya
Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kwa kipindi cha mwaka 2014,
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, James Lembeli, alisema Serikali kupitia
Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), inapoteza Shilingi bilioni mbili
kila mwezi kupitia tozo mpya kwa mfumo wa ‘fixed rate’ badala ya mfumo
wa zamani ‘Concession rate’ katika kipindi cha kuanzia Septemba mwaka
jana mpaka hivi sasa. Alisema Septemba 12, mwaka jana, Mahakama Kuu
Kanda ya Arusha ilitoa hukumu ya kesi iliyofunguliwa na baadhi ya
wamiliki wa hoteli zilizoko katika Hifadhi za Taifa dhidi ya Tanapa
kupinga Shirika hilo kuanza kutoza tozo mpya kwa mfumo huo wa fixed rate
badala ya mfumo wa zamani wa Concession rate.
“Katika hukumu hiyo mahakama iliagiza Wizara ya Maliasili na Utalii
kutoa tangazo katika gazeti la serikali kuhusu kuanza kutumika kwa tozo
mpya, ni takriban miezi minne sasa tangu kutolewa kwa hukumu hiyo,
lakini tangazo hilo halijatolewa, hali ambayo inasababisha Tanapa na
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kuendelea kupoteza mapato yanayofikia
shilingi za Kitanzania bilioni mbili kila mwezi,” alisema Lembeli.
Alisema kuwa tangu kufunguliwa kwa kesi hiyo mwaka 2011 hadi
Septemba 2014 Shirika la Hifadhi za Taifa limepoteza karibu shilingi
bilioni 80 kutokana na kukosa malipo ya tozo hiyo.
Lembeli alisema kuwa Kamati yake iliitaka Wizara ya Maliasili na
Utalii iwe imeshatoa tangazo hilo hadi kufikia Januari 28, mwaka huu,
lakini mpaka hivi sasa tangazo hilo bado halijatolewa. Akichangia
mjadala huo, Zitto alisema miongoni mwa mapendekezo ya Serikali yalikuwa
ni mashirika mawili ya hifadhi ya Tanapa na Ngorongoro yawe sehemu ya
wamiliki wa hisa za Shirika la Ndege la Tanzania ATCL ili kulikwamua
shirika hilo la ndege kwa sababu utalii na ndege vinahusiana.
Alisema Shirika la ndege ambalo kwa sasa lina hali mbaya kifedha,
linahitaji fedha za kununulia ndege mpya, lakini bado taifa linapoteza
mabilioni ya fedha kutokana na uzembe wa Waziri kwa sababu ya
kutokusanya kodi ya kwenye tozo ya utalii.
“Waziri Nyalandu yuko pale, anashindwa kutoa tangazo la Serikali,
ili kodi hii iweze kukusanywa, tutaendelea mpaka lini sisi waheshimiwa
wabunge kulalamika na kulalamika hatuchukui hatua…Mheshimiwa Spika
naomba nitoe wito kwa Bunge lako tukufu, kufika jioni ya leo (jana),
tutakapokuja kufanya majumuisho, kama tangazo la Serikali kwa ajili ya
kukusanya tozo hizi halijatoka, Waziri awasilishe barua yake ya
kujiuzulu kwa Rais,” alisema Zitto na kuongeza:
“Hatutaki kuwa na mchezo na masuala ya fedha za umma, tunalalamika
kila siku na kinachohitajika ni tangazo kwa ajili ya kukusanya all most
two billions kila mwezi, tumeshapoteza eighty billions mpaka sasa…
nakuomba tutakapofika jioni haujatoa tamko la tangazo hili, tusikuone
humu bungeni kwa sababu hatuwezi kuvumilia upotefu wa mapato ya
serikali.”
Kwa upande wake Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola, alimtaka
Waziri Nyalandu kukabiliana na mamba pamoja na viboko ambao alidai kuwa
wanaua na kuwatafuna watu ambao ndiyo wapiga kura wake jimboni badala ya
kuendelea na harakati zake za kukimbilia Ikulu.
Alisema mamba na viboko hao wanashambulia watu na kuwaua kiasi cha
kumaliza wapigakura wake huku akihoji kuwa ikiwa wapigakura wake
watakwisha ni nani atamrejesha bungeni kwenye uchaguzi Mkuu ujao
unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.
“Nilikwambia hapa bungeni kwamba wananchi wangu wa Mwibara
wanateketea kwa sababu ya mamba, viboko, lakini mpaka leo haujafika
kule, wapigakura wangu wanaendelea kutafunwa, nani atanirudisha bungeni
kama wapigakura wangu wanaendelea kuliwa na mamba wako hawa,” alihoji
Lugola.
Alisema kuwa wananchi hao wakijaribu kupambana na viboko pamoja na
mamba hao, wanakamatwa na askari kwamba wanaua wanyama ambao ni
maliasili ya taifa, lakini serikali haiwasaidii kukabiliana nao ili
wasiendelewe kuuawa.
Lugola alimtaka Waziri Nyalandu kuitisha mkutano wa mamba na viboko
waliopo katika eneo hilo na kuwazuia wasiendelee kuua watu ili kunusuru
wapigakura wake jimboni.
“Sasa nakuhakikishia, endapo hautafanya mkutano na hawa mamba na
hutafanya mkutano na hao viboko, kuwaambia wasitafune wana-Mwibara, huko
unakokimbilia, kama umeshindwa kutafuna mamba na viboko na sasa
unakimbilia Ikulu, Ikulu kule ndiko utaweza?” alisema Lugola.
NYALANDU AJIBU
Naye Waziri Nyalandu alisema baada ya hukumu, alitoa maagizo
akielekeza kuwa tangazo hilo lichapwe kwenye gazeti la Serikali kabla ya
Desemba mwaka jana.
LUKUVI
Lukuvi alidaiwa kumkingia kifua mwekezaji, ambaye amegoma kuilipa
manispaa ya Kinondoni Sh. bilioni tatu kwa ajili ya kuendeleza viwanja
vitatu vinavyomilikiwa na manispaa hiyo, jijini Dar es Salaam.
Viwanja hivyo, vipo katika eneo la Oysterbay Villa, manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Lugola ambaye aliibua tuhuma hizo, alisema migogoro ya ardhi nchini
imekuwa ni historia ya miaka mingi na kwamba, ni vigumu kwisha iwapo
viongozi wa serikali watakuwa ndiyo wahusika wakuu wa kujihusisha nayo.
Lugola alisema baadhi ya viongozi wamekuwa wakihodhi maeneo na
wengine wakiwabeba kwenye mbeleko wawekezaji, ambao baadaye huzua
migogoro baina yao na wananchi wa kawaida.
Alitolea mfano wa mwekezaji huyo, ambaye alisema historia
inaonyesha kuwa alifika katika eneo hilo na kuingia makubaliano ya
kuviendeleza viwanja hivyo.
"Na historia inaonyesha wakati mheshimiwa Lukuvi akiwa mkuu wa mkoa
(wa Dar e Salaam) ndiye ambaye alihakikisha yule mwekezaji anapata lile
eneo," alisema Lugola.
Alisema wakati Waziri Lukuvi akiwa amefanya hivyo, ndiye huyo huyo
tena amepelekwa kwenda kuongoza Wizara ya Ardhi ilihali mwekezaji huyo
bado ana mgogoro na manispaa hiyo.
"Mwekezaji yule ana kiburi, alizuia kamati ya Bunge isikanyage
ardhi ya wananchi ya Watanzania ili tuweze kuona apartment 17, manisipaa
ya Kinondoni," alisema Lugola.
Aliongeza: "Mheshimiwa Spika, mheshimiwa Lukuvi, mwekezaji yule
amehakikisha kwamba, Kinondoni hawatapata Sh. bilioni 3, ambazo
anadaiwa. Na wewe ndiye unambeba kwenye mbeleko."
"Pamoja na kwamba, mwekezaji huyo alizuia wabunge kuingia,
alijifanya ni baunsa katika nchi hii, nikamwambia hapa amefika, nchi hii
kuna mabaunsa ambao ni sisi. Nilihakikisha natumia ubaunsa wangu
kuhakikisha kumdhibiti yule mwekezaji tukaingia kwenye vile viwanja
viwili vya manispaa ya Kinondoni.
"Nakuhakikishia mheshimiwa Lukuvi ukiendelea kumbeba kwenye mbeleko
nitahakikisha naichoma moto na kuhakikisha huyu mwekezaji anadondoka."
Alihoji sababu za serikali kutumia risasi, mabomu na virungu
kuwapiga watu, kama kina Prof. Ibrahim Lipumba (Mwenyekiti wa Chama cha
Wananchi-CUF), akiwa ni mmoja wa waombelezaji waliokuwa wakiomboleza
vifo vya wenzao badala ya kutumia silaha hizo kuwatandika wawekezaji
fedhuli kama hao ili watoe fedha za Watanzania.
LUKUVI AJIBU
Akijibu hoja hizo jana jioni, Lukuvi alisema siyo yeye
aliyesababisha mgogoro huo na kwamba alichofanya ni kuingilia kati na
kuhakikisha majengo yanarejeshwa kwa Manispaa.
Alisema alihakikisha pia mkataba wa miaka 99 wa awali unarekebishwa
na kuwa wa miaka 47 na kusema kuwa mgogoro huo umekwisha na leo pande
hizo mbili zitatiliana saini.
Post a Comment