Dodoma. Wakati Rais Jakaya Kikwete akitarajiwa kutua mjini hapa
mwishoni mwa wiki hii kuendesha kikao cha Baraza la Mawaziri, huku
Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), ikitarajiwa kukutana muda wowote kuanzia
wiki ijayo kujadili pamoja na mambo mengine, mchakato wa Kura ya Maoni
na Uchaguzi Mkuu.
Chanzo chetu cha habari kilisema jana kuwa Kikwete atakuwa mjini hapa wikiendi hii kuendesha kikao cha Baraza la Mawaziri.
Hata hivyo CCM imeanza hatua ya kwanza kuelekea
Uchaguzi Mkuu wakati kikao cha NEC kikitarajiwa kufanyika mwezi huu
kupanga tarehe na utaratibu mzima wa uchukuaji na urejeshaji fomu kwa
wagombea wa chama katika ngazi za urais, ubunge na udiwani.
Tayari Rais Kikwete amepuliza kipenga cha mbio za
urais kwa CCM katika sherehe za miaka 38 ya kuzaliwa kwake wakati wa
maadhimisho yaliyofanyika mkoani Ruvuma, akiwataka wenye sifa wajitokeze
kuchukua fomu huku akisema: “Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka
huu wa kupata rais wa awamu ya tano, utakuwa wa kihistoria.”
Waliotangaza, wanaotajwa
Hadi sasa makada wa CCM waliotangaza nia kuwania
urais ni Naibu Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano, January
Makamba; Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangalla; Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.
Pia wapo wanaotajwa kwamba huenda wakajitokeza
mchakato huo utakapoanza rasmi ambao ni Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu
Nchemba; Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi; Mbunge wa
Sengerema, William Ngeleja; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe; Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta na mawaziri
wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.
Wengine ni Spika wa Bunge, Anne Makinda; Waziri wa
Katiba na Sheria, Dk Asha - Rose Migiro; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya na Waziri wa Kilimo, Chakula na
Ushirika, Stephen Wasira.
Kura ya Maoni
Katika kikao cha NEC ambacho kitakutana muda
wowote wiki ijayo inadaiwa kuwa suala la kura ya Maoni huenda likaibua
mjadala mkubwa kutokana na kuibua mijadala mingi hasa kutokana na kile
kilichoelezwa kuwa muda wa utekelezwaji wake hautoshi.
Viongozi wa vyama vya upinzani wameshatangaza kuwa hawatashiriki katika mchakato huo.
Jana, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi na Mbunge wa
Kuteuliwa, James Mbatia aliwasilisha bungeni hoja za kutaka kuahirishwa
kwa mchakato huo akisema uko nyuma ya wakati.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق