KIUNGO wa Simba ambaye alijiondoa kwenye kikosi
hicho kwa madai ya kutoridhishwa na baadhi ya mambo ya ndani ya klabu
hiyo, Shabani Kisiga jana jioni alitinga kwenye mazoezi ya timu hiyo
yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Dege Beach, Mbweni jijini Dar.
Championi lilimshuhudia Kisiga aliyekuwa amevalia mavazi ya kiraia
akitinga mazoezini hapo na baadaye akazungumza na kocha wa kikosi hicho,
Goran Kopunovic kwa zaidi ya dakika tano kabla ya kumuacha nje ya uwanja
na kwenda kuendelea na program ya kuwanoa vijana wake.
Hata hivyo baada ya mazoezi kumalizika kocha huyo alirejea na
kuungana na kocha msaidizi, Selemani Matola na kiongozi wa Simba, Salim
Swaka ambapo walionekana wakizungumza na kiungo huyo lakini inaonekana
hawakufikia muafaka kwani baada ya kumaliza viongozi hao waliondoka
pamoja tofauti na Kisiga ambaye alitimka kivyake.
Championi lilijaribu kuwahoji wahusika hao kwa nyakati tofauti
mazoezini hapo kuhusiana na kile walichokuwa wakikizungumza na Kisiga
ambapo wote waligoma kuliongelea suala walilokuwa wakilijadili.
إرسال تعليق