Maandamano ya vijana CUF yapigwa marufuku

Dar es Salaam. Licha ya Jumuiya ya vijana wa Chama cha Wananchi (CUF) kusisitiza azma yao ya kuandamana leo, polisi imepiga marufuku maandamano hayo na kusema halitosita kutumia nguvu endapo vijana wa chama hicho watakaidi amri ya kutoandamana.
Vijana wa chama hicho wamepanga kufanya maandamano leo kushinikiza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kuongeza muda wa kuandikisha wapiga kura kutoka siku saba mpaka 14. Pia, jumuiya hiyo inapinga uvunjifu wa haki za binadamu.
Januari 27, wafuasi wa chama hicho walifanya maandamano na kukabiliana na kipigo kutoka kwa polisi huku mwenyekiti wao, Profesa Ibrahimu Lipumba akikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa kosa la uchochezi na kuhamasisha maandamano hayo.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana ya chama hicho (Juvicuf), Hamidu Bobali alisema watafanya maandamano ya amani leo kuelekea Wizara ya Mambo ya Ndani na ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kupinga ukiukwaji wa haki za binadamu.
Maandamano hayo yanayoongozwa na makamu Mwenyekiti taifa, Babu Duni Haji yanatarajiwa kuanza saa mbili asubuhi kupitia Barabara za Uhuru, Bibi Titi na baadaye Barabara ya Ohio kisha kufika wizarani na ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Nec.
Bobali alisema pingamizi lililowekwa na jeshi hilo halina mashiko na kwamba hawajashawishika kuyasitisha. Aliwataka watu wote wapenda haki kujitokeza kwa wingi ili kushiriki katika maandamano hayo yatakayoanzia Buguruni Rozana.
“Tutakusanyika kuanzia saa mbili asubuhi na maandamano yataanza saa nne. Tutaanzia Buguruni-Rozana kupitia barabara ya Uhuru kisha Bibi Titi na baadaye Ohio. Tunaenda wizarani kuwaeleza mambo tunayoona kuwa hayaendi sawa.
Hakutakuwa na vurugu na hatujajipanga kupambana na polisi. Lakini endapo watatushambulia tutajilinda,” alisema Bubali.
Kwa maelezo ya CUF ni kwamba ufanisi wa mashine za BVR hautoweza kuandikisha wananchi wote wanaostahili kwa muda uliotengwa kwani zinauwezo wa kuandikisha watu 40 pekee kwa siku tofauti na inavyoelezwa na Tume kuwa ni watu 70.
Akizungumza na waandishi wa habari, kamanda wa polisi, kanda maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema wamezuia maandamano hayo kwa sababu vijana wa CUF hawana sababu za msingi za kuandamana, na waliwaambia wawasilishe madai yao Nec moja kwa moja.
Kova alisema sababu nyingine waliyoitoa kwamba wanapinga uvunjifu wa haki za binadamu haina mashiko kwa sababu suala la haki za binadamu linashughulikiwa kisheria baada ya uchunguzi kufanyika.
“Hatutakubali maandamano hayo kwa sababu tumebaini hayana lengo zuri. Tutatumia uwezo wetu kwa mujibu wa sheria kuhakikisha kuwa maandamano hayo hayafanyiki na kuleta kero kwa Watanzania wengine,” alisema.

Post a Comment

Previous Post Next Post