Dar es Salaam. Licha ya Jumuiya ya vijana wa
Chama cha Wananchi (CUF) kusisitiza azma yao ya kuandamana leo, polisi
imepiga marufuku maandamano hayo na kusema halitosita kutumia nguvu
endapo vijana wa chama hicho watakaidi amri ya kutoandamana.
Vijana wa chama hicho wamepanga kufanya maandamano
leo kushinikiza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kuongeza muda wa
kuandikisha wapiga kura kutoka siku saba mpaka 14. Pia, jumuiya hiyo
inapinga uvunjifu wa haki za binadamu.
Januari 27, wafuasi wa chama hicho walifanya
maandamano na kukabiliana na kipigo kutoka kwa polisi huku mwenyekiti
wao, Profesa Ibrahimu Lipumba akikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa
kosa la uchochezi na kuhamasisha maandamano hayo.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana ya chama hicho
(Juvicuf), Hamidu Bobali alisema watafanya maandamano ya amani leo
kuelekea Wizara ya Mambo ya Ndani na ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(Nec) kupinga ukiukwaji wa haki za binadamu.
Maandamano hayo yanayoongozwa na makamu Mwenyekiti
taifa, Babu Duni Haji yanatarajiwa kuanza saa mbili asubuhi kupitia
Barabara za Uhuru, Bibi Titi na baadaye Barabara ya Ohio kisha kufika
wizarani na ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Nec.
Bobali alisema pingamizi lililowekwa na jeshi hilo
halina mashiko na kwamba hawajashawishika kuyasitisha. Aliwataka watu
wote wapenda haki kujitokeza kwa wingi ili kushiriki katika maandamano
hayo yatakayoanzia Buguruni Rozana.
“Tutakusanyika kuanzia saa mbili asubuhi na
maandamano yataanza saa nne. Tutaanzia Buguruni-Rozana kupitia barabara
ya Uhuru kisha Bibi Titi na baadaye Ohio. Tunaenda wizarani kuwaeleza
mambo tunayoona kuwa hayaendi sawa.
Hakutakuwa na vurugu na hatujajipanga kupambana na polisi. Lakini endapo watatushambulia tutajilinda,” alisema Bubali.
Kwa maelezo ya CUF ni kwamba ufanisi wa mashine za
BVR hautoweza kuandikisha wananchi wote wanaostahili kwa muda
uliotengwa kwani zinauwezo wa kuandikisha watu 40 pekee kwa siku tofauti
na inavyoelezwa na Tume kuwa ni watu 70.
Akizungumza na waandishi wa habari, kamanda wa
polisi, kanda maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema wamezuia
maandamano hayo kwa sababu vijana wa CUF hawana sababu za msingi za
kuandamana, na waliwaambia wawasilishe madai yao Nec moja kwa moja.
Kova alisema sababu nyingine waliyoitoa kwamba
wanapinga uvunjifu wa haki za binadamu haina mashiko kwa sababu suala la
haki za binadamu linashughulikiwa kisheria baada ya uchunguzi
kufanyika.
“Hatutakubali maandamano hayo kwa sababu tumebaini
hayana lengo zuri. Tutatumia uwezo wetu kwa mujibu wa sheria
kuhakikisha kuwa maandamano hayo hayafanyiki na kuleta kero kwa
Watanzania wengine,” alisema.
إرسال تعليق