Dodoma. Umoja wa Wainjilisti wa Kikisto
Tanzania (Uwakita), umemtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda (pichani)
kuuondoa Muswada wa Mabadiliko ya Sheria vinginevyo utazunguka nchi
nzima kuwahamasisha waumini wake kuipigia kura ya hapana Katiba
Inayopendekezwa.
Wiki hii, Serikali inakusudia kuwasilisha bungeni
muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa Mwaka 2014
unaopendekeza, pamoja na mambo mengine, kufanya marekebisho kwenye
Sheria ya Tamko la Sheria ya Kiislamu, Sura ya 375.
Mapema wiki iliyopita, Jukwaa la Wakristo Tanzania
lilitoa hoja kutaka Serikali kuondoa muswada wa sheria itakayosimamia
kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi.
Hata hivyo, Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa
Kiislamu nchini imesema jukwaa hilo linaingilia madaraka ya Bunge na
kutaka Serikali ionekane inasema uongo.
Akisoma tamko hilo jana, Mwenyekiti wa Uwakita,
Samson Bullegi alisema: “Tunalitaka Bunge la Jamhuri ya Muungano
lijiepushe na mijadala ya dini, hususan suala hili la Mahakama ya Kadhi
ambalo limekuwa likijirudiarudia kila mwaka pamoja na kwamba
lilishahitimishwa na Rais,” alisema.
Bullegi alisema Uwakita unamtaka Pinda kuzingatia
mambo matatu ambayo ni pamoja na maoni ya Tume ya Kurekebisha Sheria
iliyokuwa chini ya Profesa Ibrahim Juma.
“Hakuna malumbano kati ya Waislamu na Wakristo
hapa wala Waislamu hawana malumbano na Wakristo katika jambo hili naomba
tueleweke hivyo.” alisema.
Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania (Tec), Askofu Severin Niwemugizi alisema anaunga mkono hoja za
Uwakita za kushinikiza Serikali kuondoa bungeni muswada wa mabadiliko ya
sheria akisema ni nzuri na ndiyo wanayoisimamia tangu awali akisema
hakuna msingi wa kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi kwa sababu jambo hilo
halipo pia katika Katiba Inayopendekezwa.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT),
Leonard Mtaita amepinga dhamira ya kuzunguka nchi nzima kwa madai
kwamba taasisi yao haifanyi kazi kwa maandamano, bali kuisukuma Serikali
kusikiliza hoja zao.
Msemaji wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu
Tanzania, Sheikh Rajabu Katimba alisema kinachohitajika zaidi ni elimu
ili kufahamu uendeshaji wa mahakama hiyo. Alisema Serikali inatumia
gharama kubwa kuendesha kesi, lakini baadhi ya mahakimu hawana ujuzi
katika kutatua kesi za kidini.
Post a Comment