Magu. Matukio ya ujambazi na mauaji ya kutumia silaha, yameanza kuibuka kwa kasi katika maeneo mbalimbali nchini.
Hali hiyo imekuwa ikihojiwa na wananchi na wapenda
amani na zaidi ni kuhusu intelijensia ya polisi kushindwa kugundua
mipango ya uhalifu.
Wachunguzi wa mambo wanasema kuwa kushamiri kwa
matukio hayo kunaleta hofu katika jamii huku jamii yenyewe ikilaumiwa
kwa kukaa kimya kwa watu wanaomiliki silaha kinyume cha sheria na
hutumia isivyo halali.
Hali hiyo imetokea mjini Magu, mkoani Mwanza kwa
watu wanaodhaniwa kuwa majambazi wakiwa na silaha za moto usiku wa
kuamkia jana walifunga Mtaa wa Kisesa Kata ya Kisesa, Wilaya ya Magu
mkoani Mwanza na kumuua mfanyabiashara Nestory Andrew umbali wa mita 50
kilipo Kituo cha Polisi.
Tukio hilo lilitokea saa 8:00 usiku, majambazi
hayo yalifunga Barabara ya Mwanza-Musoma kwa muda na kusababisha
taharuki kwa wakazi wa Kisesa huku milio ya bunduki ikitawala anga.
Wakizungumza na Mwananchi eneo la tukio jana,
mashuhuda walisema walianza kusikia milio mizito ya vitu kama bomu na
kwamba baada ya muda wakaona watu wakivamia duka la mfanyabiashara huyo
na kupiga risasi hewani.
Mmoja ya mashuhuda hao, Daud Mwalimu alisema “Mimi
ni fundi baiskeli hapa stendi jana (juzi) muda kama wa saa mbili usiku
nilisikia sauti ya vishindo kama bomu, lakini baada ya muda nikasikia
sauti za bunduki hewani,”
Aliongeza: “Kwa kweli tulitawanyika watu wote hapa
mtaani na kuacha mali zetu. Baada ya kutulia tulikuja kushuhudia nini
kilitokea, lakini tulikuta mtu mmoja ambaye ni mfanyabiashara hapa
Kisesa anavuja damu tulimuangalia tukamkuta amefariki.”
Shuhuda mwingine, Emmanuel Juke alisema watu hao
walifunga Barabara ya Mwanza-Musoma na kwamba, walikuwa wakipiga risasi
ovyo hewani.
Juke alisema hali ilikuwa mbaya, kwani hawakuwahi
kushuhudia tukio kama hilo na mtu aliyefariki alikuwa mfanyabiashara
maarufu Kisesa.
Mwandishi w habari hizi jana alifika Kituo cha
Polisi Kisesa ambako askari wa kituo hicho walikiri kuwapo kwa tukio
hilo huku wakitaka atafutwe Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Magu.
Kamanda w Polisi Magu, Charles Mkapa alithibitisha
kutokea kwa tukio hilo, lakini akadai msemaji mkuu ni Kamanda wa Polisi
Mwanza
- Mwananchi
Post a Comment