CCM itatua mzigo wa makosa ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa?

Machi mwaka huu Chama cha Mapinduzi (CCM) kinatarajia kuanza rasmi mchakato wake wa kura ya maoni ya kuwapata wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani watakaopeperusha bendera ya chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu.
Wahenga walisema kufanya kosa siyo kosa bali kurudia kosa. Katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vitongoji na Vijiji wa mwaka jana tumeshuhudia CCM kikifanya makosa na sasa kinayajutia.
CCM ilifanikiwa kupata ushindi wa jumla wa mitaa na vijiji 9,406, kwa pamoja vyama vingine vya upinzani, viligawana nafasi 3,211.
Kwa ushindi huo upinzani umeongeza viti 1,981 ikilinganishwa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliopita wa mwaka 2009 ambao kwa ujumla, ulipata nafasi 1,230 za wenyeviti wa mitaa na vijiji.
Kwa upande wake, CCM imepoteza nafasi 2,636 za uenyekiti wa vijiji na mitaa ikilinganishwa na uchaguzi wa mwaka 2009 ilipopata jumla ya viti 12,042.
Machi mwaka huu CCM inatarajia kuanza mchakato wake wa kupata wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi watakaosimamishwa kupambana na wale wa upinzani katika kuwania nafasi za ubunge, udiwani na hata urais.
Tumeshuhudia pilikapilika za kujipitisha kwa baadhi ya makada wenye nia ya kuwania nafasi hizo, lakini ukweli ni kwamba CCM inapaswa kuhakikisha kwamba hairudii tena kufanya makosa yaliyowanufaisha wapinzani.
Makosa ya CCM yalipoanzia
Makosa hayo ya CCM yalianzia kwenye mchakato wa kura za maoni na malalamiko ya wanachama wake yalihusu kutopitishwa kwa viongozi waliowataka, badala yake baadhi ya viongozi kutaka kutimizwa kwa matakwa yao binafsi.
Msemo wa umoja ni nguvu utengano ni dhaifu, hapo ndipo ulipodhihirika baada ya baadhi ya wanachama kuamua kujitenga kuunga mkono na kusaidia kampeni na badala yake wakaanza kuchafuana na hatimaye kutoa mwanya kwa wapinzani kushinda.
CCM ingawa imeongoza kwa kupata idadi kubwa ya viti hivyo, bado matokeo hayo yanabaki kuwa changamoto kubwa kwa sababu viti vilivyochukuliwa awali vilikuwa chini ya CCM.
Kumbe picha iliyopo hapa ni kuwa kama wapinzani watajipanga vyema, wana uwezo wa kuongeza zaidi majimbo kama walivyofanya katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
- Soma Zaidi Mwananchi Hapa

Post a Comment

Previous Post Next Post