Dar es Salaam. Wakati vyama vingine vinavyounda
Ukawa, vikiendelea na mchakato wa kutafuta jina litakalopendekezwa
kuchukua kiti cha urais, Mwenyekiti wa Chama cha NLD, Dk Emmanuel
Makaidi amesema, tayari chama chake kimeshapendekeza jina lake kuwa
miongoni mwa vigogo watakaoshindanishwa kwenye kinyang’anyiro hicho.
Ili kupatikana jina la mgombea mmoja atakayechukua
nafasi hiyo, makubaliano ya umoja huo yanaelekeza vyama kupendekeza
jina moja litakalowakilishwa katika Kamati ya Wataalamu ya Ukawa kabla
ya kushindanishwa na majina mengine.
Katika harakati za kutafuta jina la mgombea mmoja,
wenyeviti wenza wa Ukawa walikuwa wakifanya mikutano mara kadhaa na
Januari mwaka huu walifikia makubaliano ya kuanza mapema kwa mchakato
huo.
Mkutano huo ulielezwa kuwa na ajenda kadhaa
ikiwamo changamoto ya uandikishaji wa Daftari la Wapigakura, hali ya
uchumi na suala la mgombea urais kupitia umoja huo.
Hata hivyo, Vyama vya NCCR Mageuzi, CUF na Chadema
bado havijaonyesha mwelekeo wa kupatikana jina la mgombea wa urais
kutokana na michakato inayoendelea ndani ya vyama hivyo.
Jana, Dk Makaidi alisema kwamba wanachama wa chama
hicho wameridhishwa na uwezo, ushawishi wake hivyo kupendekeza jina
lake kuingia kwenye kinyang’anyiro cha urais kupitia Ukawa.
“Kwa hivyo baada ya kuungana na Ukawa, wanachama wakabariki jina langu lipelekwe kwenye umoja huo,” alisema na kuongeza;
“Mkutano uliopita tulikubaliana kwamba, jina la
mgombea mmoja wa urais kupitia Ukawa lazima lipatikane mwishoni mwa
Aprili…Makubaliano hayo yalitokana na mkutano wa wenyeviti wa Januari
mwaka huu.”
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF)
Bara, Magdalena Sakaya alisema katika mkutano huo walikubaliana mpaka
kufikia Mei, vyama vyote viwe vimekamilisha taratibu zote ili kuanza
mchakato wa kutafuta jina la mgombea urais wa Ukawa.
Katika hatua nyingine, Sakaya alikanusha taarifa
zilizoripotiwa hivi karibuni kwamba, jina la Profesa Ibrahim Lipumba
limepitishwa na chama hicho.
“Utaratibu utakaoanza kwa sasa ni uchukuaji wa
fomu za kuwania nafasi mbalimbali za urais, ubunge na udiwani kupitia
kura ya maoni ndani ya chama,” alisema na kuongeza:
“Jina la mgombea urais haliwezi kupitishwa na
kutangazwa bila kufuata kanuni…Lazima lijadiliwe kwenye vikao kuanzia
vya wakurugenzi wa chama mpaka Mkutano Mkuu wa Baraza Kuu la chama na
hatua hiyo inaweza kufanyika Mei au Aprili mwishoni.”
- Soma Zaidi Kwa Kubofya Hapa(Mwananchi)
- Soma Zaidi Kwa Kubofya Hapa(Mwananchi)
Post a Comment