Tuliangalie jimbo hili tangu mwanzo wa mfumo wa
vyama vingi. Mwaka 1995 wananchi wa Kigoma Kaskazini waliamini
watachagua upinzani, hasa NCCR –Mageuzi. Kwa bahati mbaya matokeo
yalipotangazwa, mgombea wa CCM alishinda kwa kura kidogo, huku kura zake
zikizidiwa mbali na mchanganyiko wa kura za mgombea wa NCCR-Mageuzi na
vyama vingine vya upinzani.
Mwaka 2000 mgombea wa CCM Halimenshi Mayonga
alishinda huku vyama vya upinzani vikigawana kura na kusalimu amri kwa
CCM kwa mtindo uleule wa 1995. Mara baada ya uchaguzi wa 2000 wakati,
ambapo Chadema ilikuwa ikinoa makada wenye uwezo mkubwa akiwamo Zitto
Kabwe, mapinduzi ya kifikra yalizidi kukua katika Jimbo la Kigoma
Kaskazini, huku Zitto akiendelea kujipanga wakati akimalizia masomo yake
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mwaka 2005 ulikuwa ni mwaka muhimu kwa siasa za
Mkoa wa Kigoma. Huu ni wakati ambapo Jimbo la Kigoma Kaskazini
lilimpeleka bungeni kijana wa miaka 29, huyu ni Zitto Kabwe. Zitto
alipata ushindi wa asilimia 51.1 uliotokana na kura 28,198 dhidi ya
mgombea wa CCM na mbunge aliyekuwa akimaliza muda wake Mayonga
Halimenshi aliyepata asilimia 39.6 zilizotokana na kura 21,822.
Wagombea wa CUF na NCCR-Mageuzi kwa pamoja
walipata asilimia 8.8 ya kura zote, kutokana na kura 4,824. Mwaka huo,
mwanya wa wapinzani kugawana kura na kuiachia CCM ushindi haukufua dafu
mbele ya mikakati kabambe ya Zitto na chama chake. Zitto alikuwa ‘Rafiki
wa Mbowe’ hasa na alikuwa tegemeo muhimu la Chadema.
Kipindi cha 2005–2010 kilishuhudia harakati nyingi
kwa nchi nzima kwa jumla. Pia, mmoja wa wanasiasa waliong’ara na
kufanya vyama vya upinzani vizidi kukubalika huku vijana wakianza
kujitanabaisha kama tumaini la pekee katika nchi yetu, ni Zitto Kabwe.
Zitto wakati huo akishirikiana na Dk Wilbrod Slaa wakifanya kazi chini
ya Hamad Rashid wa CUF (Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni) walifanya
kazi kubwa bungeni na nje ya Bunge. Wakati ule ungeweza kudhani kuwa
wao ndiyo walikuwa viongozi wa kambi ya upinzani bungeni.
Harakati za Zitto na wenzake katika wakati huo
naweza kusema zilikuwa chanzo cha Chadema kuaminiwa na kukua katika
majukwaa ya wananchi wa kawaida, huku vijana wengi wakijiunga na siasa
kwa kuona uthubutu mkubwa alioufanya Zitto Kabwe na wenzake.
Mwaka 2010 Zitto aligombea tena, mara hii CCM
ikimleta Robinson Fulgence Lembo na CUF ikimsimamisha mgombea mwenye
nguvu, Omary Mussa Nkwarulo. Matokeo yalipotangazwa Zitto Kabwe
aliwashinda wapinzani wake kwa kupata kura 23,366 (asilimia 48.57),
dhidi ya kura 18,352 (asilimia 38.15) za Fulgence wa CCM, huku Nkwarulo
wa CUF akipata kura 4,839 (asilimia 10.06). Ukitizama utaona kuwa
ushindi wa Zitto haukuporomoka sana, ulishuka kwa asilimia tatu tu
ukilinganisha na ule wa mwaka 2005.
Zitto amefanikiwa kuliongoza Jimbo la Kigoma
Kaskazini kwa kipindi cha pili 2010–2015 na ametangaza kutogombea tena
mwaka huu na badala yake anakwenda Kigoma Mjini ambako Peter Serukamba
wa CCM naye ametangaza kuondoka na kuja kugombea Jimbo la Kigoma
Kaskazini.
Jambo moja ambalo naliona hapa Kigoma Kaskazini ni
kuwa, Zitto akishaondoka itavipasa vyama vya Ukawa vitafute mgombea
imara ambaye anaweza kutoa ushindani mkubwa kwa Peter Serukamba ama
mbunge mwingine yoyote wa CCM. Chama cha ACT Tanzania nacho kinakuja kwa
kasi kubwa katika Jimbo la Kigoma Kaskazini na kuna wananchi wana
hasira za uhusiano mbaya kati ya Zitto na chama chake, Chadema.
Ukichanganya mambo yote hayo unaweza kuanza kuona
kila dalili ya upinzani kufanyiana vurumai na mwishowe jimbo kuangukia
mikononi mwa CCM. Kwa siasa za Kigoma jambo hilo linawezekana sana.
Hatma ya kisiasa ya Zitto itategemeana sana na karata atakazocheza ikiwa
atagombea Kigoma Mjini kama inavyosemwa.
Ikiwa kweli anakwenda Kigoma Mjini itabidi ajikaze
kisawasawa. Pamoja na kuungwa mkono katika maeneo kadhaa hapo Kigoma
Mjini, huwezi kudharau nguvu ya vyama vya Ukawa ikiwa vitaweka mgombea
mmoja kwani Zitto hawezi kugombea tena kupitia Chadema na labda atatumia
Chama cha ACT Tanzania ambacho kimefanya harakati zake nyingi mkoani
Kigoma na hata kupata matokeo muhimu katika baadhi ya maeneo kwenye
uchaguzi wa Serikali za Mitaa
- Zaidi Soma Hapa(Mwananchi)
Post a Comment