Moshi. Makatibu wa Chadema kutoka mikoa 20 ya
Tanzania Bara, wanatarajia kufanya operesheni ya kuing’oa CCM katika
Jimbo la Mwanga linaloshikiliwa na Profesa Jumanne Maghembe.
Katibu wa Chadema Mkoa Kilimanjaro, Basil Lema,
alisema jana kuwa watalishambulia jimbo hilo kama nyuki na kuliondoa
kwenye mikono ya CCM.
“Tutakutana pale kuanzia Machi 6 na baada ya
makamanda hawa kukutana, watatawanyika kwenye vitongoji vyote 282 vya
jimbo hilo kutoa mafunzo kwa viongozi wa ngazi ya chini,” alisema.
Lema alisema lengo la operesheni hiyo ni kuunga
mkono kazi iliyofanywa na Katibu wa Chadema, Mkoa wa Kinondoni, Henry
Kilawo tangu mwaka 2011 na kukiletea chama mafanikio ya kisiasa.
“Tunataka kuweka historia ya kuondoa watu
wanaotawala majimbo kifalme. Kazi tutakayoifanya ndiyo itakayofanyika
katika majimbo mengine, uzuri wao (CCM) Mwanga hawaelewani,” alisema
Lema.
Profesa Maghembe ambaye pia ni Waziri wa Maji
alipoulizwa na gazeti hili kuhusu operesheni hiyo, alisema hatishiki kwa
sababu amejenga misingi imara ya kukubalika.
“Wao waje tu kwa sababu nimewazoea kwa mbwembwe
zao mwisho wa siku wanaondoka wameinamisha vichwa chini. Mimi najivunia
rekodi yangu ya utendaji,” alisema Maghembe.
Katika hatua nyingine; Mwenyekiti
wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Philemon Ndesamburo amesema kitendo
cha Kamati Kuu cha kumuengua katibu aliyeshinda Moshi Vijijini, Emanuel
Mlaki kitakuja kukigharimu chama baadaye.
Mwaka jana, wajumbe wa Baraza la Mashauriano walimchagua Mlaki kuwa katibu kwa kura tisa, huku Akwilin Chuwa akipata nne.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika
alisema kamati imerejesha jina la Chuwa na Mlaki ataendelea kubaki kuwa
katibu wa jimbo

Post a Comment