Jumamosi iliyopita, Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), lilitangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne wa mwaka 2014.
Wanafunzi waliomaliza kidato cha nne mwaka 2014
ndiyo waliohitimu darasa la saba mwaka 2010. Mwaka huo waliofaulu
walikuwa 478,912 sawa na asilimia 53.51 ya wanafunzi 895,013 waliofanya
mtihani.
Safari yao ya kimasomo imekuwa ikiendelea huku
wakiwaacha wenzao njiani, kwani Serikali ikatangaza kuwa wanafunzi
456,350 ndiyo waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2011,
ikiwa ni sawa na asilimia 95.3 ya wale waliofaulu mtihani wa darasa la
saba.
Hii inamaanisha kuwa waliwaacha wenzao 22,562
ambao hawakuweza kuchaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka 2011.
Wengine wameishia njiani kwani ni wanafunzi 288,365pekee ndio waliofanya
mitihani ya kidato cha nne. Wanafunzi 167,985 kati ya 456,350
waliofaulu kujiunga kidato cha kwanza 2011 walipotelea njiani mpaka
sasa. Hii ni idadi kubwa .
Wakati waziri Kawambwa anasoma matokeo yao ya
darasa la saba mwaka 2010, alisema walifaulu Kiingereza kwa asilimia
36.47 na Hisabati kwa asilimia 24.70. Hii ndiyo sababu wanafunzi hawa
hawakufaulu mtihani wa hesabu kidato cha nne kwakuwa hawakuwa na msingi
bora tangu wakiwa shule ya msingi.
Ufaulu wa Hesabu umeshuka hadi asilimia 19.58
tofauti na 24.70 walizopata kwa mtihani wa darasa la saba mwaka 2010.
Hata hivyo, inaonekana ufundishaji wa Kiingereza wakiwa sekondari
uliimarika kidogo hadi kupata ufaulu wa asilimia 55.10 katika kidato cha
nne kutoka asilimia 36.47 za ufaulu wa darasa la saba mwaka 2010.
Mwaka 2014 kulikuwa na vituo vya mitihani 5419
kukiwa na nyongeza ya vituo 1064 ukilinganisha na vituo 4355 vya mwaka
2013. Miaka ya hivi karibuni, baraza limekuwa likitenganisha makundi ya
vituo kwa kigezo cha idadi ya watahiniwa.
Lipo kundi la watahiniwa wasiozidi 40 lenye vituo
2,097 na lile la watahiniwa zaidi ya 40 lenye vituo 2,322. Hii
inamaanisha kuwa shule za sekondari zimeongezeka zaidi nchini.
Matokeo ya kidato cha nne
Mfumo wa sasa wa ufaulu unatokana na asilimia 30
za maendeleo ya shule na asilimia 70 za mtihani wa mwisho. Hivyo mfumo
huu unaonyesha kuwa umechangia kwa kiasi kikubwa aina ya matokeo
yaliyotangazwa ya wahitimu wa mwaka 2014. Hebu tuchimbue zaidi tuone
kilichopatikana na tufanye tathmini zaidi.
Mwaka 2013, ufaulu ulikuwa kwa asilimia 58.25
yaani wanafunzi 235,227 walifaulu. Kiwango hiki kilijumuisha hata wale
waliopata daraja la nne. Lakini wale waliopata daraja la kwanza hadi la
tatu walikuwa 74,324 tu, ambao ni sawa na asilimia 21.09. Waliopata
daraja la nne walikuwa 126,828 na wahitimu 151,187 walipata daraja
sifuri.
Mwaka 2014 wametumia mfumo mpya wa kupanga
madaraja kwa njia ya wastani wa ufaulu (GPA). Waliofaulu daraja la
kwanza hadi la tatu kwa mfumo huu mpya ni 73,832 sawa na asilimia 30.72.
Kati ya hawa, wasichana ni 27,991 na wavulana ni 45,841.
إرسال تعليق