Baraza la Mitihani
Tanzania (Necta) limesema usahihishaji wa mitihani ya kidato cha nne
uliofanyika Novemba mwaka jana, umekamilika.
Katibu mtendaji wa
Necta, Dk Charles Msonde amesema kuwa“usahihishaji umekamilika na baraza
lipo katika uchambuzi wa kuyapanga na tutakapokamilisha tutayatangaza”.
Alipoulizwa ni lini
hasa matokeo hayo yatatangazwa, Dk Msonde alisema: “Tumemaliza
kusahihisha na mchakato wa kuyapanga ukikamilika tutawaeleza hivyo msiwe
na shaka.”
Katika kipindi cha
miaka miwili mfululizo, mwaka 2012 na 2013, Necta ilitangaza matokeo ya
kidato cha nne mwishoni mwa Februari na mwanzoni mwa Machi.
Matokeo ya Mtihani wa
Kidato cha Nne uliofanyika mwaka 2013 yalitangazwa Februari 22, mwaka
jana na 2012 yalizua gumzo kutokana na asilimia 60 ya watahiniwa kufeli.
Kwa kawaida, muhula
wa masomo kwa kidato cha tano huanza Julai, huku Machi na Aprili
mchakato wa kuwapangia shule hufanyika wakati Mei na Juni hutumiwa kwa
maandalizi kwa wanafunzi hao.
Katika matokeo ya
2013 kama ilivyokuwa katika matokeo ya mwaka 2012, shule binafsi
zilikuwa na matokeo mazuri kulinganisha na za Serikali zilizokuwa
zikitamba miaka ya nyuma.
Kwa mujibu wa Necta,
matokeo ya mwaka 2013, shule kongwe za Serikali na zile za vipaji
maalumu, zilishindwa kuingia kwenye orodha ya shule 30 bora.
Shule kongwe
kihistoria zimekuwa zikitoka kapa katika matokeo ya Mtihani wa Taifa.
Tofauti na matarajio ya wengi, shule hizo nyingi hazikuwamo hata katika
orodha ya shule 100 bora.
Baadhi ya shule hizo
ni Fidel Castro ambayo ilishika nafasi ya 83, Malangali (172), Ifunda
Ufundi (205), Jangwani (226), Bwiru (242), Songea Wavulana (257), Pugu
(325) na Azania (333).
Ikiwa ni mwaka mmoja
umekamilika tangu Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ulipoanzishwa,
taasisi ya Hakielimu ilitoa matokeo ya utafiti wake yanayoonyesha hakuna
kilichofanyika.
Kaimu Mkurugenzi wa
HakiElimu, Godfrey Boniventura alisema Serikali isitumie kigezo cha
kuongezeka ufaulu kama ishara tosha ya kuimarika kwa elimu, kwani licha
ya ufaulu huu kuonyesha kupanda ghafla, kuna changamoto nyingi katika
sekta hiyo ambazo bado hazijatatuliwa na juhudi kubwa zinahitajika.
“Mfano migogoro ya
mara kwa mara kati ya walimu na mwajiri, utoro wa walimu, ukosefu wa
maabara, vifaa vya kufundishia na tofauti kubwa iliyopo katika gharama
za utoaji elimu nchini kati ya shule za serikali na shule za binafsi,”
alisema Boniventura.
إرسال تعليق