Matokeo ya mitihani ya kidato cha nne nchini ya mwaka 2014, yanatarajiwa kutangazwa na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), Jumapili wiki hii.
Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Charles Msonde (pichani), alitoa
ahadi hiyo kama zawadi kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mpwapwa
mkoani Dodoma, kufuatia ajali ya moto iliyotokea Januari 20, mwaka huu
na kuteketeza mali zote zilizokuwa kwenye bweni la wasichana 64 wa
kidato cha tano na cha sita.
Dk. Msonde alikuwa miongoni mwa viongozi walioongozana na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (Tamisemi-Elimu), Kassim Majaliwa, kwenye ziara ya kutoa pole katika shule hiyo.
“Zawadi niliyowaandalia ni taarifa kwamba Februari 15, mwaka huu,
tutatangaza matokeo ya mitihani iliyofanywa na watahiniwa wa kidato cha
nne nchini. Nasema ni zawadi kwa sababu sijaitoa mahali kokote, nyie
ndiyo wa kwanza kuipata,” alieleza Msonde.
Watahiniwa waliotarajiwa kufanya mtihani huo Novemba, mwaka jana ni
297,488 huku watanihiwa 245,030 wakiwa wa shule na watahiniwa wa
kujitegemea walikuwa 52,448. Watahiniwa wa shule walioandikishwa ni
wavulana 132,244 (asilimia 53.97) na wasichana 112,786 (asilimia 46.03).
Kwa kawaida, matokeo ya kidato cha nne hutolewa Aprili, lakini
mwaka huu yatatoka mapema kutokana na uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka
huu. Walimu ni miongoni mwa watumishi wa serikali ambao hutumiwa
kusimamia uchaguzi mkuu.
Kupitia ziara hiyo, Serikali imepeleka vitanda 64 ambapo magodoro
64 yalitolewa na Mbunge wa Kibakwe ambaye pia ni Waziri wa Nishati na
Madini, George Simbachawene.
Pamoja na misaada hiyo, aliahidi kupeleka madaftari, mikebe ya
vifaa vya hisabati, kalamu na kumpa kila mwanafunzi aliyekuwa akiishi
kwenye bweni lililoteketea fedha taslim ili anunue vifaa binafsi ambavyo
havikupatikana kwenye misaada iliyotolewa na wasamaria wema.
Aliongeza kuwa shule hiyo itapelekewa vitabu vya aina zote kwa
kiwango cha kila mwanafunzi kuwa na kitabu chake, vitakavyonunuliwa
kutokana na Sh. bilioni 27 ambazo zimepatikana kutoka kwenye ‘chenji’ ya
ununuzi wa rada.
Pamoja na misaada ya mahitaji binafsi ya wanafunzi inayopelekwa na
watu binafsi, taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali, misaada
mingine inayoendelea kupelekwa ni vifaa vitakavyowezesha kujengwa kwa
bweni mbadala.
Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (LAPF), umepeleka mabati 92 yenye thamani ya Sh. milioni mbili.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment