MBOWE: HATUTAKUBALI KURA ZETU ZIIBWE OKTOBA


 

Chama  Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kimejipanga kuhakikisha katika uchaguzi Mkuu hawaibiwi kura.
 
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa chama hicho, Freemon Mbowe  wakati akizindua mafunzo ya Kikosi cha Ulinzi na Usalama cha chama hicho (Red Brigade), kwa vijana 200 wa  Kanda ya Kati pamoja na Kikosi maalum cha Karate.
 
“Katika  uchaguzi huu hatutaki  kulalamika tena kwamba tumeibiwa kura na tutahakikisha  tutaomba  kura kwa wananchi na tutazilinda,” alisema Mbowe.
 
Alisema endapo watakubali kuibiwa kura maana yake hawapo tayari kuongoza.
 
Mbowe aliwataka  vijana hao wa Brigade kutokukilinda chama peke yake bali pia kiwe chachu ya ulinzi kwa jamii inayowazunguka kwenye maeneo yao.
 
Alibainisha kuwa Chadema  kitaendelea kutoa mafunzo ya ulinzi kwa vijana nchi nzima.
 
"Vijana  hawa lazima wajenge moyo wa kujitolea, chama kilijengwa na watu wenye moyo huo ambao baadhi walipata madhara mbalimbali ikiwamo kupoteza maisha,” alisema Mbowe.
 
Alisema wajenge sifa ya kuwa wakombozi wa Taifa na  malipo mengine siyo lazima walipwe hapa duniani bali  watapata  kwa Mungu.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post