Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman
Mbowe ameuvunja uongozi wa chama hicho kwenye majimbo ya Ukonga na Ilala
kutokana na kutoelewana kwa muda mrefu baina ya viongozi na kutofanya
vizuri kwa chama hicho kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika
Desemba 14 mwaka jana.
Habari ambazo Mwananchi imezipata na kuthibitishwa
na Mbowe zinaeleza kuwa mwenyekiti huyo aliuvunja uongozi huo wiki
mbili zilizopita baada ya kikao cha siri na viongozi wa majimbo hayo
kilichofanyika kwenye ukumbi wa Klabu ya Billicanas iliyopo katikati ya
jiji.
Pamoja na CCM kuibuka na ushindi mkubwa kwenye
uchaguzi huo wa ngazi ya mwanzo ya uongozi, Chadema iliongoza kwa upande
wa upinzani ingawa haikuwa na matokeo mazuri kwenye majimbo hayo
mawili.
Katika uchaguzi huo, CCM ilishinda kwa asilimia
79.4 katika nafasi ya uenyekiti wa mitaa, Chadema asilimia 15.1 na CUF
asilimia 4.6. Vyama vingine kwa ujumla vilipata asilimia 0.9.
Matokeo ya uchaguzi wa wenyeviti wa vitongoji
yanaonyesha kuwa CCM ilishinda kwa asilimia 79.3, Chadema asilimia 15.6,
CUF asilimia 4.3 na vyama vingine vilipata asilimia 0.8. Katika
uchaguzi wa nafasi za uenyeviti wa mitaa, CCM ilishinda kwa asilimia
66.5, Chadema asilimia 25.4, CUF asilimia 6.8 na vyama vingine vilipata
kwa asilimia 1.3.
Matokeo ya Wajumbe wa Serikali za vijiji/mitaa
yanaonyesha CCM ilipata asilimia 79.3, Chadema asilimia 15.7, CUF
asilimia 4.3 na vyama vingine asilimia 0.7, wakati katika wajumbe wa
viti maalum CCM ilipata asilimia 82.1, Chadema asilimia 13.7, CUF
asilimia 3.5 na vyama vilivyobaki navyo vilipata asilimia 0.7.
Mbowe akerwa
Chanzo cha habari kinapasha kuwa ushindi wa CCM
katika maeneo mengi na zaidi Jimbo la Ukonga ndiyo uliomkera zaidi Mbowe
pamoja na misigano ndani ya chama.
Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, Mbowe
alikiri kufanya kikao cha uongozi ambapo pamoja na mambo mengine
waliangalia uwajibikaji, mafanikio na kushindwa kwa chama hicho katika
uchaguzi huo wa serikali za mitaa.
Alieleza kuwa, katika kikao hicho waligundua
kasoro mbalimbali katika majimbo hayo ya Ukonga na Ilala na kuafikiana
kuwa viongozi wao wawajibike kutokana na upungufu huo.
“Tulichambua kwa kina na kuona huo upungufu,
hatukuwafukuza viongozi wale, lakini viongozi walitakiwa kuwajibika
kisiasa na walijiuzulu,” alisema Mbowe.
Kwa maelezo ya Mbowe, sasa majimbo hayo yapo
chini ya Ofisi ya Kanda Maalumu ya Mkoa wa Pwani na Dar es Salaam,
ambayo inasimamiwa na Mabere Marando hadi hapo uongozi wa kikatiba
utakaporejeshwa
إرسال تعليق