Mshambuliaji mwenye kasi wa Yanga, Mrisho Khalfan Ngassa ameibuka shujaa
baada ya kuifungia Yanga mabao mawili katika mechi dhidi ya Mtibwa
Sugar.
Yanga imelipa kisasi kwa kuichapa Mtibwa Sugar kwa mabao 2-0 katika
mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar.
Katika mechi ya ufunguzi wa ligi hiyo, Mtibwa iliichapa Yanga kwa idadi
hiyo mjini Morogoro.
Kwa ushindi huo sasa Yanga imekwea kileleni kwa kuwa na pointi 25 ikiiacha Azam yenye 22, lakini ikiwa na mchezo mmoja mkononi.
Ngassa ameibuka shujaa katika mechi ya leo ameingia katika dakika ya 53 kuchukua nafasi ya Kpah Sherman aliyechemsha leo.
Dakika hiyohiyo aliyoingia, Ngassa alipiga mpira uliogonga mwamba wa juu.
Dakika mbili baadaye aliandika bao la kwanza baada ya krosi safi ya
chinichini ya Simon Msuva kumfikia Amissi Tambwe, akiwa langoni,
akashindwa kuunganisha. Yeye akaimalizia kazi hiyo.
Kama hiyo haitoshi, dakika ya 62, Ngassa alifunga bao la pili kwa
kumchambua kipa Said Nduda baada ya pasi safi ya kupenyeza ya Haruna
Niyonzima.
Baada ya bao hilo, Yanga walionekana kucheza vizuri zaidi huku Niyonzima
na Coutinho wakionyesha kutawala zaidi katikati na Msuva na Ngassa
wakizidi kuwasumbua mabeki wa Mtibwa kutokana na kasi yao kuwa kubwa.
Juhudi za beki Salim Mbonde, zilisaidia kwa kiasi kikubwa Yanga kutoongeza bao jingine.
Mara kadhaa, Mtibwa Sugar walifika langoni lakini wakashindwa kuzitumia
nafasi zake kutokana na papara za washambuliaji wake akiwemo Ame Ally
‘Zungu’.
إرسال تعليق