Mtihani mgumu Ukawa


Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju amesema madai ya wadau ya kutaka Tume Huru ya Uchaguzi, mgombea binafsi na haki ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais mahakamani, yatafanyiwa kazi iwapo Katiba Inayopendekezwa itapitishwa kwenye Kura ya Maoni Aprili 30.
Jambo hilo ni mtihani mgumu kwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambao umetangaza kususia kuipigia kura Katiba Inayopendekezwa huku ikitaka mambo hayo matatu yafanyiwe kazi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Katika mazungumzo yake na wahariri na viongozi wa magazeti yanayochapishwa na kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) ya Mwananchi, Mwanaspoti na The Citizen jana, Masaju pia alitumia takribani saa mbili kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu suala la kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi.
Akizungumza kwenye ofisi za makao makuu ya Mwananchi Communications Tabata Relini jijini Dar es Salaam jana, Masaju alisema mambo hayo ni muhimu sana katika kipindi hiki na hivyo ni muhimu kwa wananchi kupitisha Katiba Inayopendekezwa ili masuala hayo yaandaliwe utaratibu wa kutumika kwenye Uchaguzi Mkuu ujao.
Katika mkutano wa pamoja na Rais uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana, vyama vya upinzani, vikiongozwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vilitoa hoja ya kutaka mchakato wa Katiba Mpya uahirishwe hadi baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba na kwamba katika kipindi hiki Katiba ya sasa ifanyiwe marekebisho ili Tume ya Uchaguzi iwe huru, kuingiza mgombea binafsi na haki ya kupinga mahakamani matokeo ya uchaguzi wa Rais.
- Mwananchi

Post a Comment

أحدث أقدم