Mtu mmoja mwanamume, aliyetajwa kwa jina la John
Weghai amemjeruhi vibaya mke wake, Anastazia John (18) kwa kumkatakata
na mapanga kwa kile kinachodaiwa kuchelewa kwake kupata ujauzito, katika
maisha ya wawili hao waliyoanza Februari mwaka jana.
Tukio hilo la kinyama lilitokea katika Kijiji cha Mariba, Kata ya
Mriba, wilayani Tarime mkoani Mara na majeruhi huyo amelazwa katika
hospitali ya Halmashauri ya Mji ambapo ameshonwa nyuzi 67.
Akizungumzia
tukio hilo, msichana huyo alisema kuwa mumewe amekuwa akimpa matatizo
mengi katika ndoa yake kiasi cha kumkosesha amani kwa kumpiga mara kwa
mara akimtuhumu kuchelewa kupata ujauzito.
“Kwa kweli nimekuwa nikipata mateso makubwa tangu niishi na mwanaume
huyu, nimekuwa nikipigwa mara kwa mara sababu nachelewa kupata mimba na
yeye anataka mtoto.
“Naviomba vyombo vinavyotetea na kusaidia matatizo ya ukatili kama
haya viweze kusaidia watu wanaofanyiwa maana yanaondoa utu wa mtu na
kumfanya kuishi kinyonge,”alisema Anastazia.
Alisema siku hiyo alipata majeraha makubwa katika bega na titi lake la kushoto, kitu kinachompatia maumivu makubwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania
(Tamwa), Valeria Msoka, alisema wamesikitishwa na tukio hilo, akisema ni
ukatili uliopitiliza lakini wataendelea na jitihada za kupambana na
matukio ya namna hiyo katika jamii.
Alisema muda mfupi tu umepita tokea warejee kutoka wilayani Tarime
wakiwa na ugeni mkubwa wa kimataifa kupambana na masuala ya ukatili na
kutoa ujumbe kwa wananchi juu ya athari zake lakini kuna watu
hawajabadilika.
“Tulitoa maoni kwenye Katiba mpya inayopendekezwa na tunashukuru
yamepita juu ya kuangaliwa upya kwa sheria ya wanaofanya makosa ya
ukatili kwenye jamii huenda ikaja kuwa suluhisho juu ya matukio
haya,”alisema Msoka.
Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Kanda maalum ya kipolisi
Tarime/Rorya limesema mtuhumiwa bado hajakamatwa na jitihada za kina
zinaendelea kufanywa ili kuhakikisha anakamatwa na kufikishwa kwenye
vyombo vya sheria.
Kaimu Kamanda wa Tarime/Rorya, Sweetbet Njwewike alisema katika tukio
hilo lililotokea Januari 22 mwaka huu lilichelewa kutolewa taarifa
jambo ambalo limechelewesha kupatikana kwa mtuhumiwa.
Tukio hilo
limetokea siku chache tu tokea mke wa Rais wa zamani wa Afrika Kusini,
Nelson Mandela, Graca Machel kuwepo wilayani Tarime, akihamasisha
kampeni ya kuepuka ukatili kwa watoto na akina mama.
إرسال تعليق