Mkoa wa Pwani umekumbwa na maafa kufuatia mvua kubwa
zilizoyesha mapema wiki hii zikiambatana na kimbunga na radi katika
wilaya za Kibaha na Bagamoyo, kujeruhi watu 12, kubomoa nyumba 128 na
nyingine kuezuliwa paa.
Hayo yalisemwa katikati ya wiki hii na Mkuu wa Mkoa wa Pwani,
Evarist Ndikilo wakati akitoa salamu za mkoa wake kwa Makamu wa Rais,
Dk. Gharib Bilal wakati wa hafla ya uzinduzi wa barabara ya Msoga-
Msolwa yenye urefu wa kilomita 10 na ukaguzi wa mzani wa Vigwaza.
Ndikilo alisema mvua hizo zilizonyesha kwa saa mbili mfululizo
katika wilaya hizo, zimesababisha zaidi ya watu 200 kukosa mahali pa
kuishi, wengi wao wakiwa ni wa Jimbo la Chalinze lililopo wilayani
Bagamoyo.
Alisema tathimini ya awali inaonyesha katika kijiji cha Msoga,
nyumba 47, Shule ya Msingi Msoga na Ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
ya kata zimeathiriwa na mvua hizo na watu 11 kujeruhiwa.
Alisema vilevile katika kijiji cha Tonga nyumba nne zimeathirika,
kijiji cha Ngeta Kibaha Vijijini nyumba 77 na mtu mmoja kujeruhiwa.
Alisema majeruhi hao, walipelekwa katika zahanati ya Msoga na
kituo cha afya Chalinze kwa matibabu huku baadhi yao wakiruhusiwa.
Alisema majeruhi wawili baba na mtoto wake wamelazwa Hospitali ya Tumbi Kibaha kwa uangalizi zaidi wa madaktari.
Alisema Serikali ya Wilaya ya Bagamoyo na Kibaha kwa ushirikiano
na Serikali ya Mkoa zinaendelea kufanya tathimini ya maafa hayo ili
kuwasaidia waathirika ambao kwa sasa wanahifadhiwa kwa ndugu, jamaa na
jirani zao.
Kufuatia maafa hayo, Dk. Bilal alitoa pole kwa wakazi wa Kibaha na
Bagamoyo na kuahidi kuwa Ofisi yake itachangia Sh. 5,000,000
kuwasaidia.
Waziri wa Ujenzi , Dk. John Magufuli naye aliahidi kuwachangia Sh.
milioni 1 na Mbunge wa Chalinze Ridhiwan Kikwete kiasi kama hicho.
Post a Comment