Dar es Salaam. Wakati mjadala wa majina ya watu
wanaotaka kuwania urais umepamba moto, baadhi ya wasomi, wachambuzi na
wasomaji wa gazeti hili wamesema badala ya kukimbilia majina, wagombea
hao wanatakiwa kueleza jinsi gani watakavyokabiliana na ajenda 10 muhimu
kwa maendeleo ya Taifa.
Ajenda hizo kwa mujibu wa wadau wa kada mbalimbali
walioongea na Mwananchi kuhusu vipaumbele vya taifa kwa sasa, ni tatizo
la ajira, changamoto za kuinua kilimo, kutoa elimu bora, kusimamia
makusanyo ya kodi, rasilimali za taifa na kuboresha miundombinu ya
usafiri.
Wagombea hao pia watatakiwa kueleza jinsi
watakavyoondoa migogoro ya wakulima na wafugaji, matumizi sahihi ya
ardhi, mapambano dhidi ya rushwa, uhalifu na matumizi ya dawa za
kulevya, kwa mujibu wa marejeo ya habari mbalimbali yaliyofanywa na
gazeti la Mwananchi.
Kwa kawaida, vyama vya siasa huandaa ilani zake za
uchaguzi ambazo ndiyo mwongozo wa kampeni za kutafuta kura kwa wananchi
kwa ajili ya wagombea wake wa urais, ubunge na udiwani, lakini
watatakiwa kuzingatia hoja hizo muhimu.
Katika mahojiano na wadau mbalimbali, gazeti la
Mwananchi lilitaka kujua ni mambo gani ambayo wananchi “wanataka yawe
ajenda kuu kwenye kampeni za uchaguzi ili kuikwamua nchi” kutoka hapa
ilipo, na majibu yao yalionyesha suala la ajira, kilimo, afya,
rasilimali za taifa, usafiri, maji, rushwa na migogoro ya ardhi kuwa
ndiyo mambo ambayo hayajafanyiwa kazi na hivyo wanataka kusikia wagombea
watakavyokabiliana nayo.
“Kwanza tunahitaji utawala bora unaosimamia haki,
Serikali inayofanya uamuzi sahihi,” alisema mwanasheria wa jijini Dar es
Salaam, Felix Kibodya kabla ya kutaja mambo ambayo anaona yanafaa
kupewa kipaumbele.
Usimamizi wa rasilimali
Kibodya, ambaye amewahi kuwa rais wa Chama cha
Wanasheria wa Tanganyika (TLS), alisema rasilimali zikisimamiwa na
kutumika vizuri, zitalinufaisha Taifa kwa kiasi kikubwa.
“Kuna viongozi katika nchi hii waliwahi kueleza
wazi kwamba rasilimali zikibaki ardhini haziozi. Tukifanya mchezo
rasilimali hizi zitakwisha. Suala hili linaenda sambamba na
ubinafsishaji tulioufanya miaka ya nyuma, sasa ndiyo tunaaza kuona ubaya
wake,” alisema.
Alikuwa akizungumzia rasilimali kama dhahabu,
chuma, shaba, platinum, nickel, almasi, tanzanite, rubi, garnet,
emerald, sapphire na maliasili nyingine kama gesi na mafuta.
Kati ya madini hayo, dhahabu na almasi ndiyo
zimekuwa tegemeo kubwa kwa uchumi wa Tanzania, wakati kugundulika kwa
gesi na uwezekano wa kupatikana kwa mafuta kumeinua matarajio ya maisha
bora kwa wananchi na wakati fulani Rais Jakaya Kikwete aliwahi
kunukuliwa akisema “atakuwa Rais wa mwisho kuiacha nchi maskini”.
Lakini kilio kikubwa cha wadau imekuwa ni
mikataba, ambayo imeelezwa kuwa ni ya siri na hainufaishi Taifa na
badala yake inanufaisha wawekezaji na wajanja wachache
- Mwananchi Bofya Hapa
- Mwananchi Bofya Hapa

Post a Comment