Baadhi ya watu wakiangalia moja ya nyumba za
mganga wa kienyeji zilizoteketezwa kwa moto na wananchi wa vitongoji vya
Kazunzu, kijiji cha Nyambemba, kata ya Kazunzu na wa kitongoji cha
Lueseselo, kata ya Bulyaheke, wilaya ya Sengerema, mkoa wa Mwanza,
anayedaiwa kupiga ramli kwa imani za kishirikina kuwata watu utajiri.
Wananchi wa vitongoji vya Kazunzu, kijiji cha
Nyambemba, kata ya Kazunzu, wakishirikiana na wa kitongoji cha
Lueseselo, kata ya Bulyaheke, wamempiga kwa marungu, mawe na mapanga na
kisha kumchoma moto mtu ambaye bado hajafahamika, wakimtuhumu kuwa
wakala wa kuteka watoto wakiwamo walemavu wa ngozi (albino),
akishirikiana na waganga wa kienyeji wapiga ramli kwa imani za
kishirikina za kupata utajiri.
Mbali ya kumuua, wananchi hao pia wamevunja na kuchoma moto nyumba
13 zilizoezekwa kwa bati mali ya mganga wa kienyeji mwanamke mpiga ramli
mwenye umri wa miaka 40 (jina linahifadhiwa).
Hata hivyo, mganga huyo na familia yake walifanikiwa kuwatoroka wananchi hao.
Tukio hilo lilitokea jana saa saba mchana katika kijiji cha
Bulyaheke, kata Bulyaheke, baada ya wananchi kumkamata mtuhumiwa huyo
katika kijiji cha Kazunzu na kuwaongoza hadi kijiji cha Bulyaheke kwa
mganga huyo.
Richard Mangalamu baba wa mwanafunzi aliyetekwa, Winfrida (11)
anayesoma darasa la nne Shule ya Msingi Kazunzu, alisema mtuhumiwa
alimwachia mwanafunzi huyo kutokana na kumkuta ana chale mgongoni na
kifuani akidai amepoteza ubora.
Mkuu wa Polisi wa Kituo cha Wilaya ya Sengerema, Babu Sanare na
Ofisa Mtendaji wa kata hiyo, Enock Mabula, kwa nyakati tofauti
walithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Naye Diwani wa Bulyaheke, Bagadi Nyuki, akiwa eneo la tukio,
alisema chanzo cha mauaji hayo ni marehemu kudaiwa kuwa juzi alimteka
mwanafunzi wa kike anayesoma darasa la nne katika Shule ya Msingi
Kazunzu na kumvutia vichakani na kisha kumvua nguo na kumpapasa.
Inadaiwa kuwa alimuachia huru baada ya kugundua kuwa hakuwa na sifa
zinazohitajika na mganga na mwanafunzi huyo alipofika nyumbani
aliwaeleza wazazi wake na ndipo wakishirikiana na wanakijiji wenzao
walianza kumsaka mtuhumiwa na kufanikiwa kumtambua.
Inadaiwa baada ya kubanwa mtuhumiwa huyo alikiri na kujitambulisha
alikuwa ametoka kijiji cha Katoro, mkoani Geita na alikwenda Sengerema
kwa kazi ya uwakala wa kuteka watoto.
Diwani huyo alisema marehemu aliomba apelekwe kijiji jirani cha
Bulyaheke umbali wa kilometa sita kutoka Kazunzu kwa mwenyeji wake na
mdau mwenzake, Sato, lakini wapofika walikuta amekwisha kutoroka.
Wakati huohuo, mwili wa mtoto Yohana Bahati aliyeuawa kwa kukatwa
miguu na mikono, mwili wake utazikwa kesho katika kijiji cha Kataro,
mkoani Geita.

Post a Comment