Mwenyekiti UVCCM kizimbani kwa kumtwanga makonde katibu wake

Misungwi. Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Misungwi, Mkoa wa Mwanza, Mansoor Mohamed (25) amefikishwa Mahakama ya Wilaya kwa tuhuma za shambulio la kudhuru mwili.
Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Eliasha Kisura alidai kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Februari 10 saa 7:00 mchana kwa kumshambulia kwa mateke na ngumi Katibu wa UVCCM Wilaya, Nassoro Mohamed kinyume cha sheria.
Baada ya kusomewa mashtaka, mshtakiwa alikanusha na Hakimu Mfawidhi, Godfrey Mwambapa aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 25 itakapoanza kusikilizwa.
Mshtakiwa aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na  wadhamini wawili wenye mali zisizohamishika zenye thamani ya Sh700,000.
Chanzo cha ugomvi
Chanzo cha ugomvi inadaiwa ni kambi za ubunge ndani ya UVCCM wilayani humo, hali inayoonyesha Mwenyekiti wa umoja huo, Mansoor Mohamed kutofautina na Katibu wake, Mohamed Nassoro.
Mohamed inadaiwa alishtukia kikao cha makatibu wa vijana ambacho kiliitishwa na Nassoro bila kumtaarifu yeye kama mwenyekiti.
Inadaiwa Mohamed alivamia kikao hicho cha makatibu wa kata wilayani hapa, kilichokuwa kinafanyika Ukumbi wa CCM na baada ya kumhoji katibu wake sababu za kuitisha kikao bila kumpa taarifa, walianza kurushiana maneno makali na kuanza kupigana.
Akizungumza kwa simu jana baada ya tukio hilo, Mohamed alisema alipata taarifa za kikao hicho kutoka kwa wajumbe, hivyo akalazimika kwenda ukumbini kujua sababu za katibu wake kushindwa kumpa taarifa.
“Nimepokea ujumbe wa simu kutoka kwa makatibu wa UVCCM kuwa kuna kikao, mimi sina taarifa yoyote nilikwenda kufahamu sababu za kunificha taarifa hizo,” alisema Mohamed.
Mohamed alisema kinachoendelea ni suala la makambi ya wagombe ubunge kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba, kwani akiwa kiongozi wa UVCCM hawezi kukubali kuona kanuni na taratibu zikikiukwa wilayani kwake akanyamaza.

Post a Comment

Previous Post Next Post