Misungwi. Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana Chama Cha Mapinduzi
(UVCCM) Wilaya ya Misungwi, Mkoa wa Mwanza, Mansoor Mohamed (25)
amefikishwa Mahakama ya Wilaya kwa tuhuma za shambulio la kudhuru mwili.
Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Eliasha Kisura
alidai kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Februari 10 saa 7:00 mchana kwa
kumshambulia kwa mateke na ngumi Katibu wa UVCCM Wilaya, Nassoro
Mohamed kinyume cha sheria.
Baada ya kusomewa mashtaka, mshtakiwa alikanusha
na Hakimu Mfawidhi, Godfrey Mwambapa aliahirisha kesi hiyo hadi Februari
25 itakapoanza kusikilizwa.
Mshtakiwa aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza
masharti ya kuwa na wadhamini wawili wenye mali zisizohamishika zenye
thamani ya Sh700,000.
Chanzo cha ugomvi
Chanzo cha ugomvi inadaiwa ni kambi za ubunge
ndani ya UVCCM wilayani humo, hali inayoonyesha Mwenyekiti wa umoja huo,
Mansoor Mohamed kutofautina na Katibu wake, Mohamed Nassoro.
Mohamed inadaiwa alishtukia kikao cha makatibu wa vijana ambacho kiliitishwa na Nassoro bila kumtaarifu yeye kama mwenyekiti.
Inadaiwa Mohamed alivamia kikao hicho cha makatibu
wa kata wilayani hapa, kilichokuwa kinafanyika Ukumbi wa CCM na baada
ya kumhoji katibu wake sababu za kuitisha kikao bila kumpa taarifa,
walianza kurushiana maneno makali na kuanza kupigana.
Akizungumza kwa simu jana baada ya tukio hilo,
Mohamed alisema alipata taarifa za kikao hicho kutoka kwa wajumbe, hivyo
akalazimika kwenda ukumbini kujua sababu za katibu wake kushindwa kumpa
taarifa.
“Nimepokea ujumbe wa simu kutoka kwa makatibu wa
UVCCM kuwa kuna kikao, mimi sina taarifa yoyote nilikwenda kufahamu
sababu za kunificha taarifa hizo,” alisema Mohamed.
Mohamed alisema kinachoendelea ni suala la makambi
ya wagombe ubunge kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba, kwani akiwa kiongozi
wa UVCCM hawezi kukubali kuona kanuni na taratibu zikikiukwa wilayani
kwake akanyamaza.
إرسال تعليق