Mwenyekiti wa Chadema ampongeza mbunge Filikunjombe ataka wanaopinga maendeleo kuchapwa fimbo

Mbunge wa  jimbo la Ludewa  Deo  Filikunjombe akimsikiliza  kwa makini  mwenyekiti  wa chama cha  demokrasia na maendeleo (chadema)  kata ya  Kilondo Bw Edgar Kyulla  wakati  akiagiza  wananchi  wanaopinga maendeleo ya mradi wa  umeme  kijijini hapo  kuwajibishwa kwa  fimbo (picha na  Francis Godwin)

MWENYEKITI  wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kata ya  Kilondo wilaya ya  Ludewa mkoani Njombe ashauri  wananchi  wanaokwamisha jitihada za  maendeleo  zinazofanywa na mbunge wa  jimbo la  Ludewa Deo Filikunjombe (CCM) kuchapwa fimbo .
 
Mwenyekiti   huyo Bw  Edgar Kyulla alitoa agizo hilo mbele ya mbunge  Filikunjombe na  wananchi  wa kijiji  cha Kilondo  wakati wa  mkutano wa hadhara   wa  ulioambatana na uzinduzi wa mradi wa umeme  wenye  thamani ya  zaidi ya Tsh milioni 300 uliofadhiliwa na  Wakala wa Umeme Vijijini (Rea) na  kusimamiwa na kampuni za Renewable Energy Technology Development (Retdco) na Kilondo Investment.
 
Alisema  kuwa jitihada  zinazofanywa na mbunge  Filikunjombe katika  jimbo la Ludewa ni kubwa na  za  kupongezwa na si za  kubezwa na mtu  yeyote  ama  chama  chochote za siasa  katika  jimbo  hilo .
 
 " Mbunge  wetu  anafanya kazi  kubwa  sana katika kutuletea maendeleo wananchi  wa Ludewa bila  kuangalia  itikadi za  vyama  vyetu na ni  wabunge  wachache  sana  wenye  moyo kama wa  Filikunjombe ombi langu  tuungane  pamoja katika masuala ya maendeleo wapo  wachache wetu ambao  wanatangulia itikadi  za vyama hata katika mambo ya maendeleo sasa kama  mwenyekiti wa Chadema nashauri viboko vitumike kwa wapinga maendeleo bila  kujali vyama  vyao  na  mimi nitaongoza zoezi la  kuwakamata  wote wanaopinga maendeleo hapa  kijijini kwetu " alisema mwenyekiti  huyo wa Chadema


Bw Kyulla alisema wakazi wa Ludewa wanatambua kwamba mradi huo utakaolifanya eneo hilo kupata umeme kwa mara ya kwanza, umefanikiwa kupitia jitihada binafsi za Mbunge Filikunjombe
 
Chadema ambacho awali hakikuwa na nguvu kubwa Ludewa, kimefanikiwa kushinda viti kadhaa vya wenyeviti wa vijiji na vitongoji na hivyo kujiongezea nguvu zake jimboni humu.

“ Ndugu  zangu  wananchi bila  shaka mnanitambua vema kazi yangu , ninawaonya wote watakaojaribu kumhujumu mbunge  wetu jembe mheshimiwa Filikunjombe katika utekelezaji wa mradi huu,tutaonana wabaya wote mnajua kuwa maendeleo haya hayana uhusiano wowote na itikadi bali ni kwa manufaa ya kizazi chetu na  sisi  wenyewe  ni  wabunge wangapi  wamepita  bila kuleta maendeleo Ludewa ila huyu kweli ni mbunge  wa mfano kwetu lazima   tuungana pamoja ,” alisema.



Mkurugenzi mtendaji  wa kampuni ya Kilondo Investment Bw  Eric Mwambeleko, alisema mradi huo uliwasilishwa Rea ukakataliwa kutokana na vigezo kadhaa, ndipo Filikunjombe alipoingilia kati na kufanikisha kupatikana kwa fedha za mradi.
 
  Akizungumza na  wananchi hao mbunge Filikunjombe alisema Chadema ni chama cha Watanzania wanaopaswa kuheshimiwa, lakini suala la kushika dola na kuchagiza maendeleo ya nchi, linabaki kuwa la CCM hivyo lazima wananchi  kujenga umoja katika mambo ya maendeleo .

“Tuwaheshimu, tuwapende hawa wenzetu (Chadema) lakini tuhakikishe kwamba CCM inaendelea kushika dola na kuiletea nchi maendeleo,” alisema.

Hata hivyo, alisema jukumu hilo linapaswa kufanywa na wote wenye dhamana ya kuutumikia umma katika maeneo yao bila  kujali nafasi  zao katika  jamii na  kuwa  si vibaya  hata  wazee  kushiriki katika maendeleo kwa  manma ya kwenda kushauri vijana  wanapofanya kazi .
 
Pia aliwataka wakazi wa kata hiyo kushiriki kikamilifu katika kuchangia nguvu za umma kuwasaidia wataalam wanaoujenga mradi huo ili  waweze kutekeleza kwa  moyo mmoja badala ya kuwanyima ushirikiano .
 
Mradi huo unaojengwa kwenye maporomoko ya mto Kilondo, utazalisha umeme wa kilowati 50 kwa ajili ya matumizi ya wakazi wa kijiji cha Kilondo na baadaye Nsele vijiji ambavyo kimsingi bila mradi huo  uwezekano  wa  kufikiwa na umeme wa Tanesco ni vigumu  zaidi kutokana na Jografia ya  eneo hilo la Mwambao mwa ziwa nyasa .

Post a Comment

Previous Post Next Post