Polisi wadai kukamata SMG, risasi 20 mapigano ya Tanga

Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja.
Jeshi la Polisi limekamata bunduki ya SMG yenye namba 14301230, risasi 20 na magazini moja mali ya polisi Tanga vilivyokuwa imefukiwa ardhini kwenye pango walilokuwa wamejificha watu wanadaiwa kuwa ni majambazi huku katika eneo la Amboni,  jijini hapa.
 
Silaha hiyo ni miongoni mwa silaha mbili za SMG ambazo walidaiwa kuporwa askari polisi wawili waliokuwa doria  hivi karibuni jijini Tanga na watu wasiojulikana.
 
Polisi pia wanamshikilia mtu mmoja (jina limehifadhiwa) anayedaiwa kuhusika katika tukio hilo la uhalifu katika Kitongoji cha Kona Z, Amboni.
 
Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, (pichani) alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa juzi pamoja na silaha hizo kupatikana siku hiyo kwa nyakati tofauti jijini Tanga.
 
Changonja alisema kukamatwa kwa mtu huyo kulitokana na ushirikiano wa raia wema kwa Polisi ambaye baada ya kukamatwa kwake katika mahojiano aliwapeleka askari hadi ndani ya pango walipokuwa wameficha silaha hiyo.
 
“Katika eneo la kona Z ndipo tulipomkamata mtu huyo ambaye kwa sababu za kiusalama hatuwezi kulitaja jina lake na baada ya mahojiano marefu na polisi, alikubali kutupeleka walipokuwa wameficha silaha hii moja ambayo ni miongoni mwa ile iliyoibwa kwa polisi wakiwa doria,” alisema.
 
Kuhusu harufu za miili ya binadamu inayodaiwa kutoka ndani ya pango hilo, alisema ni harufu ya ngedere ambao walikufa muda mrefu ndani ya pango hilo.
 
“Hakuna mwili wa binadamu huko ndani ni ngedere ambao walikufa ndani ya pango na walijeruhiwa …lile pango linaingiza kila aina ya mnyama,” alisema Chagonja.
 
Alisema polisi wanaendelea na msako wa kuipata bunduki  nyingine aina ya SMG na risasi 40 walizoporwa askari waliokuwa doria.
 
“Nasisitiza kwamba wananchi wawe na utulivu wakati tukiendelea na operesheni ya kuwapata hawa wahalifu kwa sasa hatutataja idadi yao, lakini wajue kuwa tumewatia nguvuni tayari…na waendelee kutupa ushirikiano hasa pale wanapomwona mtu ambaye wanamtilia mashaka,” alisema.
 
Hivi karibuni Askari Polisi wawili wakiwa katika doria waliporwa SMG mbili zikiwa na risasi 60 na watu wasiojulikana jijini hapa.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

أحدث أقدم