Polisi waporwa tena SMG, risasi 30

Kamanda Leonard Paulo.
Wimbi la uvamizi na uporaji wa silaha kwenye vituo vya polisi limeendelea kushamiri safari hii likiamia mkoani Morogoro kwa kituo kidogo cha Polisi Mngeta, kilichopo Wilaya ya Kilombero, kuvamiwa na kuporwa bunduki moja aina ya SMG na magazine moja yenye risasi 30.
 
Tukio la Morogoro lilitokea juzi majira ya saa 9:30 usiku na Jeshi la Polisi mkoani Morogoro linamtafuta kijana mmoja, Emmanuel Shewele (21), kwa tuhuma za kusababisha kuvunjwa kwa kituo hicho.
 
Mbali ya silaha hizo, wavamizi hao waliiba vielelezo vya ushahidi ili kupoteza ushahidi wa kesi zake kufuatia kushtakiwa mahakamani kwa kesi zaidi ya tano.
 
Kamanda wa polisi mkoani hapa, Leonard Paulo, alitaja vielelezo kuwa ni genereta moja, viti vinne vya plastiki, redio moja aina ya sabufa, betri ya gari moja na spika moja ya redio.
 
Alisema tayari watuhumiwa watatu wamekamatwa ambao ni Ramadhani Shewele (20), Hamisi Hamidi (45) na Egnas Shewele (34), huku wakiendelea kumtafuta Emmanuel Shewele (21) wote wakiwa ni wakazi wa kijiji cha Nakaguru A, wilayani humo.
 
Kamanda Paulo alisema polisi walifuatilia tukio hilo na kufanikiwa kuvipata vitu hivyo vikiwa katika msitu wa Simbangingile umbali wa kilometa sita kutoka kilipokuwa kituo hicho cha polisi.
 
Alisema kuna uhusiano wa vitu hivyo na mtuhumiwa anayetafutwa Shawele kutokana na kwamba vilivyoibwa ni vielelezo vyake.
 
Hili ni tukio la tatu katika kipindi kisichozidi mwezi mmoja kwa vituo vya polisi kuvamiwa na kuporwa silaha baada ya uporaji kama huo kutokea Ikwiriri na Tanga.

Post a Comment

أحدث أقدم