Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amekabidhi
madaraka ya Uratibu wa Kamati ya Wakuu wa Nchi na Serikali za Afrika ya
Mazingira (CAHOSCC) kwa Rais wa Misri, Jenerali Abdel Fatteh El Sisi.
Rais Kikwete alibeba jukumu la uratibu wa CAHOSCC
miaka miwili iliyopita baada ya kifo cha aliyekuwa mratibu wa kamati
hiyo, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Meles Zenawi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu, Rais
Kikwete alikabidhi jukumu hilo Januari 31 na kuwatahadharisha viongozi
wa Afrika juu ya athari za mabadiliko ya tabia ya nchi kwenye sekta ya
kilimo barani Afrika.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa Kikwete aliwapongeza
viongozi wengine wa Afrika wakati wa mkutano wa 24 wa Umoja wa Afrika
(AU), Addis Ababa, kwa kupata mafanikio wakati wa uongozi wake.
Kikwete alibainisha changamoto mbalimbali
zinazolikabili bara la Afrika kwenye mabadiliko ya tabia ya nchi na
kutaka ushirikiano kati ya nchi zilizoendelea ambao ndiyo wachafuzi
wakubwa wa mazingira na nchi zinazoendelea kutoka Afrika.
Rais alizitaka nchi za Afrika ambazo zinaathirika
zaidi na athari za mabadiliko ya tabia nchi, kuongeza kasi katika
kuzibana nchi tajiri ili zikubali kuchangia kwa kiasi kikubwa rasilimali
za kubabiliana na athari hizo kwa sababu zinachangia asilimia 97 ya
uchafuzi wa mazingira.
“Wao wanachangia asilimia 97 kuchafua mazingira na
kusababisha mabadiliko ya tabia nchi, sisi tunachangia asilimia tatu.
Hivyo, tunawataka wabebe mzigo mkubwa zaidi katika kurekebisha hali hiyo
kuliko sisi kwa misingi ile ya wajibu wa pamoja lakini ulio tofauti,”
alisema Rais Kikwete.
Aliongeza kuwa wakati wa uongozi wake,Bara la
Afrika limeongeza uhusiano na washirika mbali mbali duniani katika
kusimamia umuhimu wa kukabiliana kwa pamoja na athari za mabadiliko ya
tabia nchi na hasa kati ya Afrika na Bara la Ulaya.
Rais Kikwete alisema mikutano ya maandalizi
iliyofanyika Malabo, Equatorial Guinea, Dar Es Salaam na katika Umoja wa
Mataifa mjini New York wakati wa Uratibu wake, ilisaidia kuweka msimamo
wa pamoja wa Bara la Afrika na kuliwezesha Bara hilo kuzungumza kwa
sauti moja wakati wa Mkutano wa Lima.
Post a Comment