Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Dodoma, Frola Mhele,
ameambia Mahakama Kuu Kanda ya Iringa kuwa aliyekuwa askari wa Kikosi
cha Kutuliza Ghasia (FFU), Pcificus Clerofas Simon, alipelekwa kwake
kuungama kumuua aliyekuwa Mwandishi wa Habari wa Kituo cha Televisheni
Chanel Ten Mkoa wa Iringa, Daud Mwangosi, (pichani) kwa bomu bila
kukusudia.
Mhele aliyasema hayo jana mbele ya Jaji wa Mahakama hiyo, Paulo, Kihwelo, wakati akitoa ushahidi wa kesi ya mauaji ya Mwangosi.
Hakimu huyo ambaye ni shahidi wa tatu, alidai kuwa mtuhumiwa huyo
alipelekwa kwake kuungama wakati akiwa Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo
Mjini Iringa.
Alidai Septemba 5, 2012 saa 7:24 mchana, polisi walimpeleka
mtuhumiwa huyo katika mahakama hiyo kwa ajili ya ungamo na kuchukua
maelezo.
Alidai mtuhumiwa huyo alimweleza kuwa amefikishwa mahakamani hapo kwa sababu anatuhumiwa kwa kesi ya mauaji.
Shahidi huyo alidai alimkagua mtuhumiwa mwilini mwake na kumkuta
akiwa na jeraha bichi kwenye mkono wake wa kulia katika kidole cha kati
kutoka mwisho na majeraha ya zamani.
Mhele alidai alipomuuliza kuwa jeraha amelipatia wapi, alimjibu
alilipata wakati bomu lilipolipuka na kwamba hakujua kama amepata jeraha
hilo.
Alidai mtuhumiwa huyo katika maelezo yake, alimweleza kuwa Septemba
2, 2012 ilitokea kazi kijiji cha Nyololo Wilaya ya Mufindi ambako
kulikuwa na mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambao
haukua rasmi.
Alidai mkutano huo hakuwa rasmi kwa sababu wafuasi wa Chadema na
viongozi wao walikaidi amri ya Polisi ya kuzuia kufanyika licha ya
kutangaziwa ilani mara tatu.
Alidai mtuhumiwa huyo aliendelea kumweleza kuwa askari waliokuwapo
kwenye eneo hilo waliamriwa kuwatawanya kwa kutumia mabomu ya machozi.
Alidai mtuhumiwa huyo alimweleza kuwa yeye na askari wengine
walisikia sauti ya askari akipiga yowe kuomba msaada na mlio mkubwa wa
kishindo, lakini yeye hakujua mlio ule ulitokea wapi.
“Mshitakiwa katika maelezo yake alieleza kuwa inawezekana ni yeye alipiga bomu bila kujua,” alidai na kuongeza:
“Baada ya kutoka eneo la tukio na kufika kambini waliitwa kwenye
mstari na kugundulika kuwa silaha aliyoibeba yeye ndiyo ilitumika kupiga
lile bomu na kumuua Mwandishi Daudi Mwangosi, lakini yeye hakukusudia.”
Shahidi wa nne, Lewis Tiekya (29) ambaye alikuwa mtunza ghala la
silaha msaidizi, alidai kuwa siku ya tukio alipokea simu kutoka kwa Mkuu
wa FFU, Said Mnunka, saa 12:30 asubuhi akimweleza kuwa anahitajika
haraka katika ghala la silaha kwa sababu kuna dharura imetokea wilayani
Mufindi.
Tiekya alidai alimwamuru atoe silaha ili kwenda kuweka amani kijijini hapo.
Alidai silaha ya mtuhumiwa iliyokuwa na namba 040824 ilirudi kama
ilivyo kwa sababu hakujua kama ndiyo imetumika kupiga bomu hilo.
Alidai wakati huo alitoka na mabomu 15 ya kishindo kikubwa na 22
ya moshi ya kurusha kwa mikono, risasi za SMG 60 ambazo hazikurudi hata
moja.
Mtuhumiwa huyo anatetewa na Wakili Rwezaula Kaijage.
Mahakama hiyo ilipokea vielelezo vya kesi hiyo ambavyo ni silaha ya
kishindo namba 040824, maelezo ya ungamo la mtuhumiwa na kitabu cha
orodha ya majina ya askari wanaochukua na kurudisha silaha ghalani.
Wakili wa Serikali Ladislaus Komanya, alidai kuwa mashahidi wawili
wameshindwa kufika kwa sababu hati ya kuitwa haikuwafikia na mmoja
ameomba udhuru kwa sababu ameuguliwa ghafla.
Komanya aliiomba mahakama kuwa ombi la pili la utuzwaji wa
kielelezo cha mashitaka namba nne ambayo ni bunduki mahakama itoe ili
itunzwe na Jeshi la Polisi hadi itakapohitajika kwenye kikao kijacho.
Komanya alidai kielelezo namba tano ambacho ni kitabu cha orodha ya
kuchukua silaha na kurudisha irejeshwe kwa upande wa mashtaka kwa
sababu inatumiwa na jeshi hilo.
Aliomba karatasi ambayo ilitumika siku hiyo kwa ajili ya kuchukua silaha, ibaki mahakamani hapo kwa ajili ya ushahidi.
Wakili Kijage hakuweka pingamizi kuhusu kielelezo namba nne kutunzwa na polisi, kadharika na kielelezo namba tano.
Hata hivyo, aliomba shauri lipewe kipaumbele katika kikao kijacho kwa sababu mtuhumiwa yupo rumande.
Mwangosi aliuawa Septemba 2, mwaka 2012 katika kijiji cha Nyololo,
wilaya ya Mufindi wakati akiwa kwenye majukumu yake ya kazi kwenye
mkutano wa Chadema wa kufungua tawi la chama hicho.
Jaji Kihwelo aliahirisha kesi hiyo mpaka Msajili wa Mahakama
atakapopanga kikao kijacho kutokana na mashahidi wengine watatu kutofika
mahakamani kutoa ushahidi.
إرسال تعليق