Serikali
imeelezea kusikitishwa na uamuzi wa Kenya wa kuzuia magari ya kitalii
ya Tanzania kwenda kuchukua na kushusha watalii wanaotumia Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, kwa kusema kuwa hatua hiyo haijengi
wala kuendana na dhamira njema ya mkataba wa kuanzisha Jumuiya ya
Afrika Mashariki (EAC).
Maeneo
hayo ni pamoja na miji ya mipakani na miji rasmi iliyopendekezwa na
kukubalika na pande zote mbili ikiwemo Nairobi ambako Kiwanja cha Ndege
cha Kimataifa cha Jomo Kenyatta kipo.
Waziri
wa Afrika Mashariki, Dk Harrison Mwakyembe alisema jana kuwa, dhamira
ya kuanzishwa upya kwa jumuiya hiyo haiendani na tukio la aina hiyo.
Hata
hivyo alisema kwamba Serikali ya Tanzania itaendelea kuheshimu na
kuzingatia amri iliyotolewa na Kenya ili kulinda undugu na urafiki
uliopo kati ya nchi hizo huku wakitafakari hatua za kuchukua kuondoa
bughudha iliyotokea kwa watalii na wasafiri wanaopitia uwanja huo.
Waziri
Mwakyembe alieleza kwamba Serikali ya Tanzania itaendelea na mchakato
ulioanzishwa wa kuhusisha wadau wote wanaoguswa na tatizo hilo hadi
kufikia uamuzi ambao utauwasilisha kwa Serikali ya Kenya kupitia vikao
rasmi vya Jumuiya.
Hata
hivyo, alisema pamoja na kwamba amri hiyo ya Serikali ya Kenya
inakwenda nje ya mkataba wa 1985 kwa kuvihusisha hata viwanja vya ndege
kuwa sehemu ya vivutio vya utalii, Serikali ya Tanzania itaheshimu na
kuzingatia amri hiyo ili kulinda undugu na urafiki uliopo kati ya nchi
hizo mbili.
Alisema
pia kwamba Serikali itatafakari hatua za kuchukua ili kuondoa bughudha
kubwa itakayotokea kwa watalii na wasafiri wanaokuja nchini wanaopitia
uwanja huo wa Jomo Kenyatta.
Alizitaja
hatua hizo kuwa ni pamoja na kuwafahamisha watalii na wageni wote wenye
nia ya kutembelea vivutio vya kitalii vya Tanzania kutumia viwanja
vingine vya ndege ili kuepuka kadhia na gharama zisizo za lazima.
Waziri
huyo alisisitiza kuwa viwanja vya ndege hasa vile vya kimataifa
vitaendelea kuwa sehemu ya milango ya kuingilia na kutokea kwenda kokote
ndani ya Jumuiya au nje ya Jumuiya na havitachukuliwa kama vivutio vya
utalii.
"Tanzania
haitazuia magari ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki au
nchi nyingine yoyote kuingia katika viwanja vyake vya ndege kuleta au
kuchukua watalii wanaopitia katika viwanja hivyo na kwenda katika nchi
zao," alisema.
Dk
Mwakyembe ambaye ni Waziri mpya kwenye wizara hiyo alisema mkataba wa
mwaka 1985 kati ya Tanzania na Kenya ulilenga kutoa mwongozo wa
ushirikiano katika Sekta ya Utalii kati ya nchi hizo mbili.
Aliongeza
kuwa makubaliano hayo yalielekeza maeneo muafaka kwa ajili ya
kubadilishana watalii huku ikizingatiwa kuondoa bughudha kwa watalii.
Post a Comment