Tanzania Yasikitishwa na Uamuzi wa Kenya wa kuzuia magari ya kitalii ya Tanzania

Serikali imeelezea kusikitishwa na uamuzi wa Kenya wa kuzuia magari ya kitalii ya Tanzania kwenda kuchukua na kushusha watalii wanaotumia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, kwa kusema kuwa hatua hiyo haijengi wala kuendana na dhamira njema ya mkataba wa kuanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Waziri wa Afrika Mashariki, Dk Harrison Mwakyembe alisema jana kuwa,  dhamira ya kuanzishwa upya kwa jumuiya hiyo haiendani  na tukio la aina hiyo.
 
Hata hivyo alisema kwamba Serikali ya Tanzania itaendelea kuheshimu na kuzingatia amri iliyotolewa na Kenya ili kulinda undugu na urafiki uliopo kati ya nchi hizo huku wakitafakari hatua za kuchukua kuondoa bughudha iliyotokea kwa watalii na wasafiri wanaopitia uwanja huo. 
 
Waziri Mwakyembe alieleza kwamba Serikali ya Tanzania itaendelea na mchakato ulioanzishwa wa kuhusisha wadau wote wanaoguswa na tatizo hilo hadi kufikia  uamuzi ambao utauwasilisha kwa Serikali ya Kenya kupitia vikao rasmi vya Jumuiya.
 
Hata hivyo, alisema pamoja na kwamba amri hiyo ya Serikali ya Kenya inakwenda nje ya mkataba wa 1985 kwa kuvihusisha hata viwanja vya ndege kuwa sehemu ya vivutio vya utalii, Serikali ya Tanzania itaheshimu na kuzingatia amri hiyo ili kulinda undugu na urafiki uliopo kati ya nchi hizo mbili.
 
Alisema pia kwamba Serikali itatafakari hatua za kuchukua ili kuondoa bughudha kubwa itakayotokea kwa watalii na wasafiri wanaokuja nchini wanaopitia uwanja huo wa Jomo Kenyatta. 
 
Alizitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kuwafahamisha watalii na wageni wote wenye nia ya kutembelea vivutio vya kitalii vya Tanzania kutumia viwanja vingine vya ndege ili kuepuka kadhia na gharama zisizo za lazima.
 
Waziri huyo alisisitiza kuwa viwanja vya ndege hasa vile vya kimataifa vitaendelea kuwa sehemu ya milango ya kuingilia na kutokea kwenda kokote ndani ya Jumuiya au nje ya Jumuiya na havitachukuliwa kama vivutio vya utalii. 
 
"Tanzania haitazuia magari ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki au nchi nyingine yoyote kuingia katika viwanja vyake vya ndege kuleta au kuchukua watalii wanaopitia katika viwanja hivyo na kwenda katika nchi zao," alisema.
 
Dk Mwakyembe ambaye ni Waziri mpya kwenye wizara hiyo alisema mkataba wa mwaka 1985 kati ya Tanzania na Kenya ulilenga kutoa mwongozo wa ushirikiano katika Sekta ya Utalii kati ya nchi hizo mbili. 
 
Aliongeza kuwa makubaliano hayo yalielekeza maeneo muafaka kwa ajili ya kubadilishana watalii huku ikizingatiwa kuondoa bughudha kwa watalii. 
 
Maeneo hayo ni pamoja na miji ya mipakani na miji rasmi iliyopendekezwa na kukubalika na pande zote mbili ikiwemo Nairobi ambako Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Jomo Kenyatta kipo.

Post a Comment

أحدث أقدم