Elizabeth Edward na Emma Kalalu,Mwananchi
Dar es Salaam.Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
(TCRA) imewataka viongozi wa dini kutumia nafasi kukemea juu ya matumizi
mabaya ya mitandao ya kijamii kwa waumini wao na kuelimisha madhara
yanayoweza kusababishwa na teknolojia hiyo katika jamii.
Hatua hiyo ya TCRA imekuja kufuatia kukithiri kwa
vitendo vinavyoashiria kutumika vibaya kwa mitandao ya kijamii kama njia
ya mawasiliano hali inayochangia kuzidi kuporomoka kwa maadili.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Profesa John Nkoma alisema
lengo la kukutana na viongozi hao ni kuwapa elimu kuhusiana na madhara
ambayo jamii inaweza kupata kufuatia ongezeko la matumizi mabaya ya
mitandao.
“Mitandao ni mizuri sana lakini tatizo ni jinsi
inavyotumika watu wamekuwa wakifanya mambo ya ajabu tena bila kuwa na
hofu ya Mungu ndiyo maana tumerudi kwenu viongozi wa dini mtusaidie
katika hili:
Kwa kutumia nafasi zenu tuna imani mtawaelimisha
waumini ili waelewe kuwa kusambaza ujumbe unaoashiria uchochezi ni kosa
kisheria na inaweza kuwa dhambi kwani hakuna ambaye angependa amani
ivunjike”
Katika miaka ya hivi karibuni baada ya kuboreshwa
na kurahisishwa kwa teknolojia ya mawasiliano watu wamekuwa wakitumia
mwanya huo kusambaza meseji na picha za matusi na zinazolenga kuleta
uchochezi.
Alisema ili kuepukana na madhara inawalazimu
watanzania kuachana na matumizi mabaya ya mitandao na badala yake
kuitumia katika kuleta maendelea kwenye sekta mbalimbali ikiweo
elimu,biashara na uchumi.
“Vijana watumie mitandao kujifunza mambo
mbalimbali yanayoweza kuwa na manufaa kwao na taifa lakini sio
kuhamasishana vitu vya ajabu”alisema.
Kwa upande wake Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam Alhadi Mussa Salum aliwataka watanzania kuwa makini na matumizi
ya mitandao na kusisitiza kwamba inaweza kusababisha madhara makubwa kwa
taifa.
Naye Askofu Msaidizi wa kanisa la KKKT huku
akiwasisitiza kuzingatia hofu ya Mungu katika kila wanalofanya hali
itakayowaweka mbali na vitendo viovu.
Post a Comment