Dar es Salaam. Waliokuwa wafanyakazi 10 wa Chama cha Wanasheria
Wanawake Tanzania (TAWLA) wamefungua kesi ya madai Tume ya Usuluhishi
na Uamuzi (CMA) dhidi ya Mkurugenzi Mtendaji wa chama hicho, Tike
Mwambipile.
Katika kesi hiyo, inayosikilizwa na Hakimu Gerald
Jumanne, wafanyakazi hao wanadai kuwa wamefungua kesi hiyo ya madai
baada ya Mwambipile kuwafukuza kazi bila ya kufuata utaratibu na
kushindwa kuwalipa stahiki zao.
Mwanasheria anayemtetea Mwambipile katika kesi
hiyo, Mary Richard alidai kuwa yeye hana nguvu ya kisheria kwa sababu
mwanasheria aliyetafutwa na TAWLA kusimamia kesi hii yupo safarini hivyo
aliomba iahirishwe.
“Mheshimiwa Hakimu mimi sio sio Mwanasheria
mwenye dhamana ya kusikiliza kesi hii kwani wanamsubiri mwanasheria
mwingine aliyetafutwa na chama hicho kwa ajili ya kuendelea kusikiliza
na kwamba barua ya wito tumeletewa Jumatatu hivyo isingekuwa rahisi kwa
leo kuanza kusikilizwa kwa shauri hilo”alisema Mary.
Mwanasheria huyo aliendelea kudai mahakamani hapo
kuwa madai yaliyopo kwenye kesi hiyo dhidi ya Mkurugenzi Mtendaji wa
Tawla hayana mashiko na akasisitiza iahirishwe hadi tarehe nyingine
kwa ajili ya kufanya usuluhishi.
Wafanyakazi hao katika madai ya msingi wanadai
kuwa walifukuzwa bila ya utaratibu kufuatwa na hawakulipwa stahiki zao
na nafasi zao zilitangazwa na kupewa watu wengine kinyume na makubaliano
yao.
Walidai kuwa baada ya kufukuzwa kazi, Mkurugenzi
Mtendaji huyo aliwaahidi kuwarejesha kazini kwa kuwataka waombe tena
nafasi zao kupitia tangazo lililotolewa Oktoba 2014, na Novemba Mosi,
2014 ajira mpya ilianza lakini wao hawakuwemo.
Tume hiyo ya Usuluhishi na Umauzi, Februari
12,2015 itasuluhisha mgogoro uliopo baina ya watu hao 10 waliokuwa
wafanyakazi wa TAWLA dhidi ya Mkurugenzi Mtendaji wa chama hicho.
Post a Comment