Mkurugenzi Tawla aburuzwa mahakamani

Dar es Salaam.  Waliokuwa wafanyakazi 10 wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) wamefungua kesi ya madai Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) dhidi ya Mkurugenzi Mtendaji wa chama hicho, Tike Mwambipile.
Katika kesi hiyo, inayosikilizwa na Hakimu Gerald Jumanne, wafanyakazi hao wanadai  kuwa wamefungua kesi hiyo  ya madai baada ya Mwambipile kuwafukuza kazi bila ya kufuata utaratibu na kushindwa kuwalipa stahiki zao.
Mwanasheria anayemtetea Mwambipile katika kesi hiyo, Mary Richard alidai kuwa  yeye hana nguvu ya kisheria kwa sababu mwanasheria aliyetafutwa na TAWLA kusimamia kesi hii yupo safarini hivyo aliomba iahirishwe.
 “Mheshimiwa Hakimu mimi  sio sio Mwanasheria mwenye dhamana ya kusikiliza kesi hii kwani wanamsubiri mwanasheria mwingine aliyetafutwa na chama hicho kwa ajili ya kuendelea kusikiliza na kwamba barua ya wito tumeletewa Jumatatu hivyo isingekuwa rahisi kwa leo kuanza kusikilizwa kwa shauri hilo”alisema Mary.
Mwanasheria huyo aliendelea kudai mahakamani hapo kuwa madai yaliyopo kwenye kesi hiyo dhidi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Tawla  hayana mashiko na akasisitiza iahirishwe  hadi tarehe nyingine kwa ajili ya kufanya usuluhishi.
Wafanyakazi hao katika madai ya msingi wanadai kuwa walifukuzwa bila ya utaratibu  kufuatwa na hawakulipwa stahiki zao na nafasi zao zilitangazwa na kupewa watu wengine kinyume na makubaliano yao.
Walidai kuwa baada ya kufukuzwa kazi, Mkurugenzi Mtendaji huyo aliwaahidi kuwarejesha kazini  kwa kuwataka waombe tena nafasi zao kupitia tangazo lililotolewa Oktoba 2014, na Novemba Mosi, 2014 ajira mpya ilianza lakini wao hawakuwemo.
Tume hiyo ya Usuluhishi na Umauzi,  Februari 12,2015  itasuluhisha mgogoro uliopo baina ya watu  hao 10 waliokuwa wafanyakazi  wa  TAWLA  dhidi ya Mkurugenzi Mtendaji  wa chama hicho.

Post a Comment

أحدث أقدم