Tufunguke tusiburuzwe na vyama katika chaguzi

Tumeufikia mwaka wa uchaguzi. Ni mwaka wa furaha kwa wengine kwani wameishi kwa matumaini ya kupata nafasi za uongozi kwa kipindi wanachojua wao na hivyo mwaka huu ni mwaka wao wa kujaribu bahati yao.
Ni mwaka wa kihoro kwa wengine haswa wale waliopita kipindi kilichopita kwa kutoa ahadi ambazo hata asilimia moja ya ahadi hizo hazijatekelezwa, hivyo wana wasiwasi kama wapiga kura watawapa ridhaa tena. Wanasiasa kwa wakati huu hawalali, wanahaha kutafuta namna ya kuwafanya wapiga kura wawaamini na kuwapa kura zao.
Kuna mikakati ya mgombea mmoja mmoja na kuna mikakati ya pamoja kwa kiasi kikubwa ikiwa chini ya vyama vyao. Kwamba kila mtu anajitahidi kuonesha kwamba chama chake ndicho haswa kinachotakiwa kupewa ridhaa ya wananchi.
Kelele ni nyingi sana za kipi chama bora. Na sisi wapiga kura tumeunganishwa kwenye kelele hizo hizo hata tunajisau kwamba kitakachotuhudumia siyo nembo ya chama bali ni watu watakaosimamishwa na chama kile.
Tumeunganishwa katika kelele hizo kiasi kwamba hatujali tena nani tunamchagua ili mradi tu awe ametoka katika chama kile ambacho kelele zake zimetuvutia zaidi. Tunavutiwa na hizo kelele kiasi kwamba hata pale wanapotutusi kwa kutuambia kwamba chama chao hata kikisimamisha jiwe litachaguliwa tu, tunapiga makofi ya furaha kwa kauli hiyo na kweli tunalichagua jiwe lilisimamishwa. Tumeshuhudia watu wa ajabu ajabu wakiingia katika nafasi mbalimbali ambao mwisho wa siku tunagundua hawana mchango wowote katika kuboresha maisha yetu.
Jamani hebu tubadilike na kuwachagua viongozi kwa ajili yetu. Tujitathmini maamuzi tuliyoyafanye katika chaguzi za serikali za mitaa zilizopita karibuni, tuwaangalie kama wanatosha na kama hawatoshi tujiulize walipataje nafasi?
Kama kweli mwanasiasa alifanikiwa kukushawishi kumchagua mtu asiye na uwezo kwa kelele za kukiunga mkono chama basi ujue unaishi katika karne ambayo viumbe vilivyokuwepo wakati huo vyote vimetoweka na kuwekwa katika kitabu cha historia yaani wewe hupashwi kuishi katika ulimwengu huu wa leo.
Utashawishikaje kuchagua uozo wakati unajua fika kwamba huyo unayemchagua unamchagua kwa ajili ya kukuondolea maumivu yako ya; kukosa maji, kukosa zahanati, kukosa usafiri, kuzingirwa na vibaka katika eneo lako na mengine mengi. Kwa nini maumivu hayo yasiwe ndiyo mwongozo wako wa kusema mtu nitakayemchagua ni yule ambaye anaelekea kwanza kuyafahamu maumivu hayo na pia anaonesha ana mbinu za kupunguza kama siyo kuondoa maumivu hayo? Na tufunguke na kusema hatutarudia makosa tuliyoyafanya katika chaguzi zilizopita.
Tujikumbushe ulaghai tuliopewa wakati wa chaguzi za serikali za mitaa hapa karibuni na hata chaguzi nyingine za nyuma na kuweka misimamo yetu ya watu wanaotufaa. Tukumbuke kwamba ofisi za bunge, udiwani n.k siyo kituo cha ushauri nasaha kwamba mtu mwenye tabia zisizokubalika akiingia pale atapewa ushauri na kuacha tabia zake mbaya. Hivyo tunapochagua mtu tuchague yule ambaye tayari ametengenezeka. Jamii yetu ya kitanzania ina watu wenye uelewa na uwezo wa kuwahudumia wananchi kwa nini tusiwashawishi watu hao waingie kwenye kinyang’anyiro na tuwahakikishie ushindi? Au ni kwa kuwa mara nyingi watu hao wanakuwa hawana mpango wa kutukirimu?
Tuwe makini na watu wanaokuja na hoja za kwamba wamegundua kuna mapungufu haya na yale katika uongozi wa mtu ambaye kwa wakati huo yuko madarakani. Tuwashukuru waibua mabaya na kuyaweka hadharani kwani wanasaidia kutuonesha wale wanaotufilisi na kutufanya tuishi katika maisha duni. Kwa hilo tuwaambie asante na ikiwezekana tuwazawadie kwa kazi hiyo. Lakini kamwe hilo lisiwe ndiyo kigezo namba moja cha kuwapa nafasi za kutuongoza katika maeneo yetu. Sisi tunachokihitaji ni mtu mwenye uwezo wa kutupunguzia au kutuondolea maumivu yetu basi.
Ni ukweli kabisa kwamba hao wanaotafuna rasilmali zetu wanachangia kwa kiasi kikubwa kutuongezea makali katika yale ambayo kwa sasa tunaumia lakini bado nasema haiwezekani kumpa mtu nafasi kwa sababu tu amefanikiwa kumshika mwizi lakini hana sifa nyingine yoyote ya kutuongoza. Tuwaombe wale wanaokuja kujinadi kwamba pamoja na kutupa taarifa ya wezi wa nchi hii watuambie namna wao wanavyoweza kutupunguzia maumivu yetu. Ile kumkamata mwizi na kumwanika hadharani kunaonesha uzalendo, pengine hata uadilifu kama huyo msemaji naye hana tabia hizo lakini bado hakutoi kiongozi bora. Uadilifu pekee haufanyi mambo yaende; tunahitaji mtu ambaye ana uwezo wa kuzilinda hizo rasilmali lakini kikubwa awe na ubunifu wa kuzitumia kwa namna ambayo utaleta maendeleo katika jamii zetu.
Tukilaghaiwa kuchagua watu ambao kila kunapokucha kazi yao ni kusema tu nani kaiba, nani kaficha basi tujue kuna uwezekano mkubwa kwa watu hao kuendelea kututajia watu waliotuibia bila kutupa suluhu yoyote ya matatizo yetu kwa kipindi chote cha miaka mitano. Na hapa naomba nieleweke vizuri kwamba sijaribu hata kidogo kuwaponda wanaoibua wezi la hasha. Ninachotaka nieleweke ni kwamba anayetaka uongozi asiegemee tu kwenye ujasiri wake wa kuwataja wezi hadharani kwani hiyo ni sifa ya ziada; anahitajika kuwa na sifa zitakazochangia katika kuondoa kama siyo kufuta kabisa kero zetu kwani ubora ndio tunda tunalotaka kuliona.

Post a Comment

Previous Post Next Post