Dar es Salaam. Wananchi wengi hawana uelewa wa
kutosha juu ya taasisi za Serikali za ukaguzi wa hesabu na jinsi
zinavyofanya kazi ya kusimamia fedha za Umma, utafiti uliofanywa na
Twaweza umebainisha.
Taasisi hizo ni pamoja na Ofisi ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC) na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).
Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo leo, jijini
Dar es Salaam, Mtafiti wa Twaweza, Constantine Manda amesema ni
mwananchi mmoja tu kati ya watatu ameshawahi kusikia kuhusu CAG, na mtu
mmoja tu kati ya sita anaweza kueleza shughuli za CAG.
Manda amesema mwananchi mmoja kati ya wanne
amewahi kusikia kuhusu PAC na LAAC na mmoja kati ya kumi anaweza
kuzielezea vema taasisi hizi. Aliongeza kuwa makundi ya wasomi, watu
wenye kipato kikubwa na wanaume waliohojiwa ndiyo walionekana kuwa na
taarifa zaidi kuhusu ofisi hizi.
“Wananchi wengi ambao hawazifahamu taasisi hizi
hawakuweza kukumbuka mafanikio yoyote yaliyopatikana ndani ya ofisi hizo
tatu katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita,” alifafanua mtafiti
huyo.
Katika utafiti huo, Twaweza iliwahoji watu 1,474
kwa njia ya simu, na kuwauliza maswali saba ili kupima uelewa wao wa
masuala ya rushwa, taasisi za ukaguzi wa hesabu na usimamizi wa fedha za
umma.
Wananchi waliulizwa kama wanaamini kuwa taasisi za
ukaguzi wa hesabu ziko huru na kama wanaamini rushwa ipo Serikalini.
Watu wawili kati ya watatu wamesema hawaamini kuwa taasisi za ukaguzi wa
hesabu ziko huru.
Pia, wananchi tisa kati ya 10 wanaamini rushwa ipo
Serikalini. Manda amesema wananchi hao wanaamini kuwa makampuni hutoa
rushwa kwa viongozi wa serikali ili kushinda zabuni au mikataba.
Hata hivyo, Manda amesema asilimia 34 ya wananchi wanaamini kuwa aina hii ya rushwa huandikwa na kuonekana kwenye ripoti ya CAG.
“Watanzania wanaamini kuwa rushwa hairipotiwi
kikamilifu kwa kiwango inachotendeka. Wengi wanapendekeza ripoti ya CAG
kusambazwa kwenye redio kwa kuwa ndiyo njia yenye ufanisi zaidi,”
ameongeza Manda.
Walipoulizwa nani anapaswa kuchukua hatua juu ya
matokeo ya ripoti ya CAG, wananchi sita kati ya 10 wanatarajia Rais
achukue hatua dhidi ya vitendo vya rushwa. Ni mwananchi mmoja tu kati ya
20 anaamini kuwa kamati za usimamizi PAC na LAAC zinatakiwa kuchukua
hatua.
“Kadhalika, wananchi saba kati ya 10 wanatambua
kuwa rushwa ni upotevu wa fedha zao. Tulitumia ripoti ya CAG ya mwaka
2012/13 kuelezea masuala ya ubadhilifu yaliyojitokeza, watu nane kati 10
wanaamini matukio hayo yanawaathiri kwa kiwango fulani,” ameeleza
mtafiti huyo.

Post a Comment