Z’bar/Dar. Chama cha Wananchi (CUF) jana
kilionyesha jinsi kilivyojiandaa kwa “mwaka wa uamuzi” wakati kilipogawa
vifaa mbalimbali vya kusimamia kuwezesha wanachama wake kusimamia
Uchaguzi Mkuu katika mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na maelfu ya watu
kwenye Uwanja wa Mnazi Mmoja.
CUF, moja ya vyama viwili vikubwa visiwani
Zanzibar, iligawa magari kwa kila wilaya na kamati zilizoteuliwa
kusimamia uchaguzi, pikipiki aina ya Vespa kwa majimbo yote 50 na katibu
mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharrif Hamad alisema lengo la mgawo
huo ni kuutangazia umma kuwa “huu ni mwaka wa uamuzi”.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa uzinduzi
wa Kamati za Uchaguzi za chama hicho kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja,
Maalim Seif alisema safari ya uchaguzi tayari imeanza na CUF imejipanga
vizuri kuliko chaguzi zote zilizopita na imeamua kutumia miezi minane
iliyobakia kukamilisha mkakati wa ushindi.
Alisema kuzinduliwa kwa kamati hizo za Uchaguzi
Mkuu ni kuanza safari ya Zanzibar kupata mamlaka kamili na kuongeza
“hakuna kuremba ni kazi, kazi, kwa sababu Wazanzibar wanaitegemea CUF
kuwakomboa”.
Alisema wamejipanga, wamejizatiti kwa kila hali
wala hakuna kinachowatisha na azma ya kutimiza wanachokitaka itatimia
kwa umoja wao.
CUF imekuwa ikitoa upinzani mkubwa katika kila
uchaguzi tangu kurejeshwa kwa mfumo wa siasa za vyama vingi, na CCM
imekuwa ikipata ushindi wa tofauti ndogo ambao mara zote umekuwa
ukilalamikiwa, hali iliyosababisha vyama hivyo kuunda Serikali ya Umoja
wa Kitaifa baada ya machafuko kutokea mwaka 2005.
“Sitaki visingizio, nimewapa vitendea kazi;
magari, pikipiki, mashine za kutolea nyaraka mbalimbali, mashine za
matangazo (PA) sasa kafanyeni kazi huku mkiyakumbuka maazimio yetu ya
mwaka huu ambayo ni kazi kwa kwenda mbele. Huu siyo mwaka 2005, wala
2010. Huu ni mwaka 2015, mwaka tofauti kwa chama chetu,” alisema Maalim
Seif.
Maalim Seif, ambaye alihutubia kwa zaidi ya saa
moja na nusu, aliamsha shangwe na vigeregere kutoka kwa watu
waliohudhuria mkutano huo wa uzinduzi wakati aliposema kuwa wanaungana
na tamko la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kutoshiriki katika
upigaji Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa.
Katibu Mkuu huyo alisema kuwa katika kuhakikisha
huu ni mwaka wa uamuzi na siyo wa uchaguzi, wananchi wa Zanzibar
wasishiriki kuipigia kura Katiba Inayopendekezwa kwa sababu siyo yao
badala yake wajipange kuhakikisha Chama hicho kinashika dola.
“Wamepiga ngoma wenyewe, wamecheza wenyewe,
tuwaache waipigie kura wenyewe. Katiba hiyo ni ya Dodoma na itabaki
huko,” alisema Maalim Seif.
Alisema wananchi wamechoka kutawaliwa na utawala
usio na upeo, dira, uadilifu, ubunifu, na mwelekeo, chama
kisichojiamini, kinachoshindwa kusimama kidete kutetea masilahi ya
Wazanzibari.
Alifafanua kuwa CUF ipo tayari na imejipanga kwa
ajili ya kutetea masilahi ya wananchi wote, kufanya uamuzi ndani ya
Zanzibar badala ya kufanyia Dodoma.
- Zaidi Hapa Mwananchi
- Zaidi Hapa Mwananchi
Post a Comment