Mikoani. Baada ya kumalizika mkutano wa 18 wa
Bunge Jumamosi iliyopita, wabunge wengi wamekimbilia kwenye majimbo yao
hatua inayohusishwa na homa ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Tofauti na kawaida ya wabunge wengi ambao baada ya
vikao vya Bunge hukimbilia Dar es Salaam, safari hii wengi wameelekea
majimboni kuweka mikakati ya kuhakikisha wanarudi bungeni katika
uchaguzi huo.
Hivi karibuni gazeti hili liliandika habari kwamba
wakati mkutano wa Bunge ukiendelea, wabunge wengi walikuwa Dodoma
kimwili lakini kiakili walikuwa majimboni.
Baadhi ya wabunge waliohojiwa jana wameelezwa kuwa
wako katika mikakati mbalimbali ya kupambana na wapinzani wao
watakaojitokeza kuwania nafasi hiyo.
Mkoani Tanga kwa mfano, wabunge karibu wote tayari wapo katika majimbo yao.
Mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM), Stephen Ngonyani
jana alikuwa kwenye mazishi ya rafiki yake na taarifa zinasema kwamba
baada ya mazishi hayo ataendelea na shughuli zake za jimbo.
Mbunge wa Tanga Mjini (CCM), Omar Nundu, Mbunge wa
Lushoto (CCM), Henry Shekifu, Mbunge wa Mkinga (CCM), Dastan Kitandula,
Mbunge wa Muheza (CCM), Herbert Mtangi wapo majimboni mwao wakiendelea
na shughuli zao.
Imeelezwa pia kwamba wabunge Yusuph Nassir
(Korogwe Mjini - CCM), Saleh Pamba (Pangani - CCM) wako Dar es Salaam
wakijipanga kurudi majimboni mwao kufanya mikutano na shughuli zao za
kisiasa.
Mkoani Iringa Mbunge wa Mufindi Kusini (CCM),
Mendrad Kigola amerejea jana asubuhi jimboni kwake akitokea Dodoma
akisema atakuwa na ratiba ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali jimboni
mwake.
Katibu wa Mbunge wa Mufindi Kaskazini, Baptist
Mdede alisema bosi wake ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii, Mahamoud Mgimwa anatarajia kurejea jimboni kwake kati ya
Februari 17 na 18.
Wabunge wengine katika majimbo ya mkoa huyo bado
hawajawasili kutokana na shughuli mbalimbali wanazofanya nje ya majimbo
yao na Mkoa wa Iringa.
Mkoani Kilimanjaro, wabunge wawili wa kuchaguliwa kati ya tisa walikuwa wamerejea majimboni baada ya kuahirishwa kwa Bunge.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق