Dar es Salaam. Siku moja baada ya Mwenyekiti wa
CCM, Rais Jakaya Kikwete kudokeza kuwa atakayekuwa mgombea wake wa
urais baadaye mwaka huu ni yule ambaye hajajitokeza mpaka sasa, makada
wa chama hicho waliotangaza nia ya kugombea urais wamesema wana uwezo na
sifa za kugombea nafasi hiyo, huku wasomi wakija na mtazamo tofauti.
Makada hao waliotangaza nia, kwa nyakati tofauti
walisema kauli hiyo haina maana kuwa Rais Kikwete anawapinga, bali
inalenga kuwataka makada zaidi wa chama hicho tawala wenye uwezo
wajitokeze na kutangaza nia ya kugombea ili waweze kupimwa uwezo wao na
Watanzania.
Juzi, wakati akihutubia katika sherehe za miaka 38
ya kuzaliwa kwa chama hicho mjini Songea, Rais Kikwete alisema, wapo
watu wenye sifa zote za urais lakini hawajitokezi na hata wakiambiwa
kuwa wanaweza husema hawajajiandaa, kwamba hao ndiyo wanaohitajika.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo wakati ambao baadhi
ya makada wa CCM wakiwa wameanza kupita huku na kule kutafuta uungwaji
mkono, huku baadhi yao wakiwa wamepewa onyo kutokana na kushiriki
kampeni kabla ya muda na kushiriki vitendo ambavyo ni kinyume na
maadili.
Ukiacha wale wanaotajwa, wanasiasa waliotangaza
nia ni Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba, Waziri wa
Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Mbunge wa Nzega, Dk Hamis
Kigwangalla na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Akizungumza jana, Makamba alisema: “Ujumbe wa
mwenyekiti uko wazi, kwamba hadi sasa hakuna ambaye anaweza kusema
anaongoza katika mbio hizi na ni sahihi kabisa kwamba bado hatuna
mgombea.
“Kitendo cha kugombea ni cha kijasiri kwa sababu
unatengeneza maadui wengi kwa hiyo kuna watu ambao wanapata woga. Ujumbe
wa Mwenyekiti umesaidia kuondoa woga kwa wale ambao hawajajitokeza.”
Dk Kigwangalla alisema: “Kila mtu ana mtazamo wake
kuhusu suala hili la urais. Siwezi kushangaa kauli ya Rais Kikwete kwa
sababu hivi karibuni wakati akiwa mkoani Tabora na Dodoma alizungumza
suala hili, kuwataka vijana kujitokeza kugombea uongozi na mimi ni
kijana nimetumia nafasi.”
“Unajua wapo waliodhani kuwa Rais Kikwete ana
upendeleo na anataka vijana wachukue nafasi hiyo. Binafsi nadhani kauli
hii ya Rais sasa itafungua ukurasa mpya, hata kwa wale ambao wameshapita
umri wa ujana nao kutangaza nia,” alisema.
Kauli ya wasomi
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Bashiru Ally
alisema: “Uchaguzi unahusisha ushindani na ushindani huo usiishie
kutazama sifa za wagombea tu, pia utazame sifa za vyama wanavyotoka,
ajenda ya vyama hivyo na historia zake.”
- Mwananchi
- Mwananchi
Post a Comment